Algeria: Uingiliaji kijeshi Libya unapasa uwe katika fremu ya sheria za kimataifa
-
Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria amesema kuwa uingiliaji wowote wa kijeshi na oparesheni dhidi ya magaidi huko Libya unapasa kutekelezwa katika fremu ya sheria za kimataifa.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Jumapili hii, Ramtane Lamamra Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria ameashiria mashambulizi ya anga ya karibuni ya Marekani dhidi ya ngome za kundi la kigaidi la Daesh huko Libya ambapo raia kadhaa wameuawa wakiwemo wanadiplomasia wawili wa Serbia na kueleza kuwa mapambano dhidi ya ugaidi huko Libya yanapasa kufanyika katika kalibu ya sheria halali za kimataifa na kuzingatia usalama, uthabiti na mamlaka ya kujitawala nchi hiyo.
Ijumaa iliyopita ndege za kivita za Marekani zilizishambulia ngome za kundi la Daesh huko Libya na kuuwa watu wasiopungua 40. Ramtane Lamamra Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria pia kwa mara nyingine tena amesisitiza umuhimu wakutumiwa njia za kisiasa kuipatia ufumbuzi migogoro yote ya kieneo.