Niger katika maombolezo ya kitaifa kufuatia kuuawa wanajeshi wake
Rais wa Niger ametangaza siku mbili za maombolezo ya kitaifa kote nchini humo kufuatia kuuliwa wanajeshi wake kadhaa katika shambulio la watu wenye silaha walioivamia kambi moja inayowahifadhi raia wa Mali katika eneo moja kaskazini magharibi mwa Niger.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Rais wa Niger imeeleza kuwa nchi hiyo inatangaza siku mbili za maombolezo ya kitaifa kufuatia kuuliwa wanajeshi wake 22 katika shambulio lililofanywa Alhamisi iliyopita na wenye silaha wasiofahamika kwenye kambi inayowahifadhi raia wa Mali katika eneo la Tazalit karibu na mkoa wa Tassara kaskazini magharibi mwa Niger.
Wizara ya Ulinzi ya Niger imetangaza kuwa wanajeshi wake 22 wameuawa Alhamisi iliyopita na watu wenye silaha na wengine watatu wamejeruhiwa. Moustapha Ledru Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Niger amesisitiza kuwa kundi hilo lililofanya shambulizi limekimbilia upande wa Mali na kwamba hadi hivi wanaendelea na msako ili kuwatia mbaroni na kuwapokonya silaha wavamizi hao.
Afisa mmoja wa idara ya usalama ya Niger ameeleza kuwa shambulizi hilo dhidi ya kambi ya wakimbizi limefanywa na watu waliokuwa na silaha wanaokadiriwa kuwa 30 hadi 40 ambao walikuwa wakizungumza lugha ya Kituareg.