Wito watolewa kuzingatia zaidi haki za watoto barani Afrika
Sambamba na kufanyika kikao cha dharura cha Umoja wa Afrika (AU) nchini Togo, mashirika ya kutetea haki za watoto yametoa wito kwa umoja huo kutenga bajeti ya fedha ya kushughulikia zaidi haki za watoto katika nchi za bara hilo.
Kundi moja la mashirika ya kutetea haki za watoto limetoa wito huo jana huko mjini Lome, Togo huku Umoja wa Afrika ukijiandaa na kikao cha dharura cha siku tano kinachotazamiwa kuanza leo na kuendelea hadi tarehe 15 mwezi huu.
Kikao hicho kitajadili masuala ya usalama wa baharini na maendeleo barani Afrika ambapo mashirika kadhaa ya kimataifa yanatazamiwa kuhudhuria likiwemo shirika la Mfuko wa Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), Mpango wa Kimataifa wa Togo, Ardhi ya Watu na taasisi ya kutetea haki za watoto ya WAO-Afrique.
Isselmou Boukhary, mwakilishi wa UNICEF na msemaji wa mashirika hayo ya kutetea haki za watoto amesema, watoto milioni 385 duniani wanaishi chini ya mstari wa umasikini wa pato la chini ya dola mbili kwa siku ambapo zaidi ya nusu ya watoto wao wanaishi katika nchi za eneo la kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika.
Kwa mujibu wa wawakilishi wa mashirika hayo ya kutetea haki za watoto, kikao cha dharura cha Umoja wa Afrika kinachoanza leo katika mji mkuu wa Togo, Lome ni fursa mwafaka ya kuchunguza haki za watoto na kutenga bajeti ya fedha kwa ajili ya kuwasaidia na kuinua hali zao za maisha.../