UN: Maelfu ya Wasomalia wakimbia mapigano, mvua zinatishia maisha yao
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, zaidi ya watu elfu 75 wamekimbia makazi yao na wengine 18 wameuawa katika wiki tatu za mapigano yanayoendelea nchini Somalia.
UN imetahadharisha kuwa, wanawake na watoto wadogo wanaolala mbungani na maeneo ya wazi wanakabiliwa na matatizo makubwa zaidi husuan kwa kutilia maanani msimu unaokaribia wa mvua kali.
Taarifa hiyo ya Umoja wa Mataifa imetolewa kufuatia mapigano makali ya Jumamosi na jana Jumatatu kati ya makundi hasimu ya maeneo mawili tofauti yenye mamlaka ya ndani ya Puntland na Galmudug katika mji wa Galkayo.
Umoja wa Mataifa unasema woga wa kuendelea mapigano hayo kwa kipindi kirefu umewalazimisha raia wengi kukimbia makazi yao na kwamba idadi kubwa ya wakimbizi hao ni wanawakwe, watu wazima na watoto.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa, mvua zinazotarajiwa kuanza kunyesha katika maeneo hayo zitawaathiri zaidi wakimbizi hao husasun wale wanaoishi katika mbuga na maeneo ya wazi.
Mji wa Galkayo ambao ni makao makuu ya mkoa wa Mudug ulioko kaskazini kati mwa Somalia umegawanywa sehemu mbili kati ya wanamgambo wa koo mbili zinazohasimiana.