Bakwata: Watanzania kunufaika na bidhaa zenye nembo "Halal"
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18121-bakwata_watanzania_kunufaika_na_bidhaa_zenye_nembo_halal
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limesema kila Mtanzania karibuni hivi atanufaika na bidhaa zenye nembo ya Halal, ambapo wapo mbioni kuijumuisha nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwenye orodha ya nchi 33 ambazo zinatumia bidhaa halali za vyakula na vinywaji.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Oct 25, 2016 04:40 UTC
  • Bakwata: Watanzania kunufaika na bidhaa zenye nembo

Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limesema kila Mtanzania karibuni hivi atanufaika na bidhaa zenye nembo ya Halal, ambapo wapo mbioni kuijumuisha nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwenye orodha ya nchi 33 ambazo zinatumia bidhaa halali za vyakula na vinywaji.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar-es-Salaam hapo jana, Katibu Mkuu wa Bakwata Selemani Lolila, amesema nembo ya Halal itaweza kumhakikishia mlaji Muislamu  na asiyekuwa Muislamu uhakika wa chakula tangu kilipotoka hadi kilipofikia.

Nembo ya Halal

Amesema kama tunavyomnukuu: "Kitabu cha Qur’ani kinatueleza kuwa tuchinje na tule vyakula halali, lakini kwa sababu mbalimbali tumekuwa tukila chakula bila kujua kimeanzia wapi na kimepita katika njia gani."

Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania ameongeza kuwa, “Kwa kutambua mchango wa dini yetu, tumepata mafunzo kutoka kwa viongozi wa jumuiya ya JAKIM ya Malaysia ambao ndio wamiliki wa nembo ya Halal na baada ya mwaka mmoja, watakuja kufanya ukaguzi wa kile walichotuachia ili kupata nembo hiyo itakayotusaidia kuuza bidhaa zetu katika nchi za Asia na nyinginezo."

Vyakula vilivyotiwa nembo ya Halal

Kwa upande wake Mkurugenzi wa jumuiya ya Halal Tanzania, Muhsin Hussein, amesema mafunzo waliyopatiwa ni ya bidhaa zinazozalishwa nchini ambazo zitatoa fursa ya kuuzwa nje ya nchi.

Alisema kwa sasa wanatarajia kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari ili waweze kuupasha habari umma katika suala zima la kutumia bidhaa zilizowekwa nembo ya Halal.