Maadui wa ash Shabab wateka mji Somalia
Maafisa wa serikali wa Somalia wamethibitisha habari iliyosema kuwa, kundi moja la wapinzani wa ash Shabab ambalo linaliunga mkono kundi la kigaidi la Daesh, limeteka mji mmoja wa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Gazeti la Le Figaro la nchini Ufaransa limewanukuu maafisa hao wa Somalia wakithibitisha habari hiyo na kusema kuwa, baada ya mapigano makali yaliyotokea leo kati ya kundi hilo na askari wa serikali, hatimaye wafuasi hao wa Daesh na maadui wa ash Shabab wameuteka mji wa Qandala wa kaskazini mashariki mwa Somalia.
Mohamed Khuurshe, afisa mwandamizi wa jeshi la polisi la Somalia katika eneo la Jamac amesema kuwa, wanajeshi wa serikali walikuwa wachache sana kwenye eneo hilo, hivyo wameshindwa kukabiliana na wanamgambo hao.
Habari zinasema kuwa, wakazi wengi wameukimbia mji huo, na hivi sasa hakuna mawasiliano yoyote na eneo hilo. Shuhuda mmoja ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, ameona kwa macho yake kundi hilo likiwa limebeba bendera na ISIS na kuingia katika mji wa bandari wa Qandala.
Naye Said Ali, mmoja wa maafisa wa polisi wa eneo la Puntland la kaskazini mashariki mwa Somalia amesema kuwa, hii ni mara ya kwanza kwa wafuasi wa genge la kigaidi la Daesh kuteka mji nchini Somalia.
Kundi hilo la wafuasi wa Daesh linaongozwa na Abdiqadir Mumin katika eneo hilo la Puntland. Abdiqadir Mumin alikuwa mkuu wa zamani wa kundi la kigaidi la ash Shabab ambaye amekata uhusiano wake na genge hilo na kujiunga na kundi jingine la kigaidi la Daesh.