Wanachama 10 wa genge la kigaidi la ash-Shabab waangamizwa Somalia
Wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la ash-Shabab nchini Somalia, wameangamizwa na jeshi la serikali kwa kushirikiana na askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika AMISOM, kusini mwa nchi hiyo.
Osman Sheikh Ali, mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya Somalia amevitaarifu vyombo vya habari kuwa, magaidi hao wameangamizwa katika operesheni zilizotekelezwa na jeshi la serikali karibu na mji wa Bardira, kusini mwa nchi hiyo. Sheikh Osman Ali ameongeza kuwa, katika operesheni hizo, wanachama wengine wapatao saba wa kundi hilo maarufu kwa kutenda jinai dhidi ya binaadamu, wamejeruhiwa.
Jeshi la serikali ya Somalia kwa kushirikiana na askari wa AMISOM limefanikiwa kuudhibiti mji huo wa Bardira kutoka mikononi mwa magaidi hao. Katika siku za hivi karibuni, wapiganaji wa kundi hilo wamekuwa wakidhibiti miji kadhaa ikiwemo ya kistratijia, baada ya askari wa AU na wale wa serikali kuondoka katika miji hiyo, na hivyo kufanya shughuli za askari wa AMISOM nchini Somalia kuwa ngumu.