Machafuko yaibuka Morocco baada ya kuuawa muuza samaki
Maelfu ya watu nchini Morocco wameandamana katika miji kadhaa baada ya muuza samaki kusagwa na kufa ndani ya lori za kuzoa takataka katika mji wa kaskazini wa Al Hoceima.
Taarifa zinasema muuza samaki huyo aliuawa wakati akijaribu kuchukua samaki wake aliokuwa akiwauza ambao walichukuliwa na polisi na kutupwa katika gari hilo la kuzoa taka. Mauaji hayo ya mchuuzi huyo wa samaki siku ya Ijumaa yamepelekea kuibuka maandamano ya wananchi waliojawa na ghadahabu dhidi ya kile walichokitaja kuwa ni, 'Hogra', istislahi ya Kimorocco inayomaanisha udhalimu rasmi wa serikali.
Maandamano hayo yameitishwa na wanaharakati wa Harakati ya Februari 20 ambayo iliandaa maandamano mwaka wa 2011 wakati wimbi la mwamko wa Kiislamu lilipooenea katika nchi za Kiarabu.
Katika hatua ya kujaribu kutuliza hali ya mambo, Mfalme Mohamed, ambaye hivi sasa yuko katika safari ya kuzitembelea nchi kadhaa za Kiafria, ameamuru waziri wa mambo ya ndani kutembelea familia ya mchuuzi huyo na kumpa salamu maalumu za rambi rambi kutoka kwa Mfalme.
Maandamano hama hayo ni nadra sana nchini Morocco, ambako mfalme bado anatawala kiimla. Morocco ilituliza maandamano ya mwamko wa Kiislamu mwaka 2011 kwa kufanya marekebisho ya kisiasa ili kuzuia kuanguka serikali kama ilivyoshuhudiwa Tunisia, Misri na Libya.
Mchuuzi huyo aliyetambuliwa kama Mouhcine Fikri alikuwa amenunua sakamaki bandarini kabla ya kupokonywa na polisi baada ya wakuu wa eneo hilo kupiga marufuku uuzaji wa baadhi ya samaki.