Viongozi wakuu serikalini wakana kuhusika na ufisadi Kenya
Waziri wa zamani wa Ugatuzi nchini Kenya, amesema baadhi ya wanasiasa mashuhuri kutoka muungano unaotawala wa Jubilee walihusika na ufisadi wa shilingi milioni 791 zilizopotea kutoka kwenye hazina ya NYS.
Bi. Anne Waiguru amesema kwenye kiapo chake kwamba, kiongozi wa wabunge wengi kwenye Bunge la Taifa, Aden Duale na seneta mashuhuri, Kipchumba Murkomen wamehusika na ufisadi wa mamilioni ya fedha katika kitengo cha huduma ya vijana kwa taifa (NYS). Waiguru amesema wawili hao pamoja na Faruq Kibet, msaidizi wa Naibu Rais William Ruto walikuwa wakitoa vitisho dhidi ya maafisa wa NYS wakati sakata hilo lilipofichuliwa na uchunguzi kuanzishwa.
Duale na Murkomen wamezungumza na waandishi wa habari mapema ljana na kusisitiza kuwa hawana hatia. Wawili hao wamemtuhumu Anne Waiguru kuwa anataka kusababisha mpasuko ndani ya muungano unaotawala wa Jubilee. Wamesema kuwa wako tayari kuchunguzwa ili ukweli ubainike.