Ujerumani kuwakamata wahamiaji baharini na kuwarejesha Afrika
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ujerumani imetoa pendekezo la kuwakamata wahamiaji Waafrika katika Bahari ya Mediterranean na kuwarejesha Afrika kabla hawajafika Ulaya.
Kwa mujibu wa toleo la leo Jumapili la gazeti la Kijerumani Welt am Sonntag, Ujerumani inataka kutumia mbinu inayotumiwa na Australia ya kuwakamata wahamiaji waliorundikana ndani ya boti baharni na kuwapelekea katika nchi nyingine kuwakagua.
Gazeti hilo limemnukulu msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ujerumani akisema kuwa lengo la uamuzi huo ni kuwapokonya motisha wahajiri ili wasituhubutu kufunga safari hatari na ghali ya kujaribu kufika katika pwani ya Ulaya.
Kwa mujibu wa mpango huo, wahajiri wanaokamatwa wakiwa ndani ya boti katika Bahari ya Mediterranean, ambao wengi hutumia pwani ya Libya kusafiria, watapelekwa Tunisia, Misri na nchi zingine za Afrika Kaskazini ili maombi yao ya ukimbizi yachunguzwe.
Karibu wahajiri 2,200 waliokolewa katika Bahari ya Mediterranean siku ya Jumamosi pekee na miili 10 kupatikana katika oparesheni ya Gadi ya Pwani ya Italia.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM linasema hadi sasa wahajiri 159,496 wamefika katika pwani ya Italia kwa boti ambapo 4,220 wengine wamepoteza maisha wakijaribu kuingia Ulaya kwa njia hiyo ya Bahari ya Mediterranean.