Rais wa Zambia asisitiza kutatuliwa changamoto zinazolikabili eneo
Rais Edgar Lungu wa Zambia amesisitizia udharura wa kutatuliwa changamoto za nchi za bara la Afrika kwa ushiriki wa asasi zote za kiraia hususan wanawake.
Rais Lungu aliyasema hayo Jumanne ya jana ambapo pamoja na mambo mengine aliongeza kuwa, usalama na uthabiti wa kisiasa na kiuchumi wa nchi za Kiafrika unategemea ushiriki wenye taathira chanya wa raia wote hususan wanawake. Amefafanua kuwa, katika hali ambayo bara la Afrika linakabiliwa na changamoto nyingi, utatuzi wake unahitajia ushiriki chanya kupitia mipango iliyoratibiwa kwa ajili ya harakati za kimaendeleo ili kufikia malengo.
Kabla ya hapo Rais wa Zambia alisisitiza juu ya udharura wa wanasiasa wote kuzingatia mazingira ya sasa ya kijamii sanjari na kujiepusha na mivutano na kuvuruga utengamano. Itafahamika kuwa, Zambia ni moja ya nchi za Kiafrika ambazo katika miaka ya hivi karibuni zimekumbwa na changamoto mbalimbali za kisiasa na kiusalama. Uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Agosti mwaka huu nchini humo ulilisukuma taifa hilo kwenye migogoro ya kikaumu na kiusalama.