Watu wenye silaha waua askari watano wa Niger
(last modified Wed, 09 Nov 2016 02:38:30 GMT )
Nov 09, 2016 02:38 UTC
  • Watu wenye silaha waua askari watano wa Niger

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Niger imetangaza kuwa watu waliokuwa wamejizatiti kwa silaha nzito wakiwa wamepanda pikipiki na vipando vingine wamevamia kijiji kimoja na kuua askari askari watano karibu na mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Mali.

Shambulio hilo la jana katika kijiji cha Banigabou kilichoko kilomita zipatazo 12 kutoka mpakani limejiri huku kukiwepo hofu ya kuenea uasi na mashambulio ya makundi ya kigaidi na kitakfiri katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa wakaazi wa kijiji hicho, ufyatulianaji wa risasi uliendelea kwa muda masaa mawili kabla ya mapambazuko.

Askari wa jeshi la Niger

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Niger haikutaja utambulisho wa washambulio hao lakini inafahamika kuwa makundi ya kigaidi na kitakfiri yenye makao yao katika eneo la jangwani kaskazini mwa Mali yamekuwa yakisonga mbele upande wa kusini kuelekea mji mkuu wa nchi hiyo kupitia mipakani katika eneo tete la Sahel.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa askari watano waliuawa na wanne wa gadi ya taifa walijeruhiwa na kwamba washambuliaji wawili pia waliuawa katika shambulio hilo. Aidha watu 26 waliokuwa wamejipenyeza kijijini humo walikamatwa wakiwa na zana na silaha za kijeshi.

Kundi la boko Haram la Nigeria linafanya mashamulio pia ndani ya Niger

Niger inakabiliwa pia na mashambulio ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram la nchini Nigeria kutokea kusini katika mpaka  wa pamoja na nchi hiyo na vilevile inakabiliwa na uwezekano wa kumiminika ndani ya ardhi ya nchi hiyo wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitaklfiri la Daesh kupitia kaskazini katika mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Libya.../

Tags