Wasiwasi kuhusu kuenea umasikini Afrika
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema umasikini ni adui mkubwa wa watu wa eneo la Maziwa Makuu barani Afrika.
Joseph Kabila aliyasema hayo Jumatano mjini Kinshasa alipohutubu katika ufunguzi wa Kongamano la uwekezaji katika sekta binafsi ya Nchi za Eneo la Maziwa Makuu. Akizungumza katika kikao hicho ambacho pia kilihudhuriwa na Ban ki-Moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kabila alisema: "Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, eneo la Maziwa Makuu Afrika limekumbwa na migogoro na ghasia jambo ambalo limepelekea kuenea umasikini miongoni mwa watu wa eneo."
Katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na wawakilishi wa nchi za eneo la Maziwa Makuu, Kabila alisema kuna haja ya kuwa na jumuiya moja ya kiuchumi ya nchi za eneo hilo.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka kuhitimishwa vita na machafuko katika eneo hilo. Amesema kukosekana amani kumetoa pigo kubwa kwa nchi hizo za Kiafrika na kuongeza kuwa, haitoshi kutatua matatizo ya kiusalama bali kuna haja ya kuwepo ustawi wa kiuchumi na kijamii ili uthabiti upatikane.
Eneo la Maziwa Makuu Afrika linajumuisha nchi za Burundi, Malawi, Rwanda, Uganda, Zambia, Tanzania, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kenya.
Umasikini na njaa ni matatizo mawili sugu yanayowakumba wakaazi wengi wa dunia hasa barani Afrika. Watu wengi Afrika wamekuwa wakikumbwa na matatizo ya njaa na ukosefu wa amani.
Mgogoro wa kisiasa Burundi, ukosefu wa usalama mashariki mwa Kongo, mivutano ya kisiasa Uganda na Rwanda ni kati ya matatizo ya eneo hilo la Afrika. Kutokana na matatizo hayo, kumeibuka idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani na nje ya eneo hilo sambamba na kuongezeka njaa na umasikini.
Katika upande wa pili, kujishughulisha vyama tawala na ukandamizaji wa wapinzani na waasi ni mambo ambayo yamepelekea bajeti za nchi hizo kutumika katika masuala ya kijeshi na kiusalama badala ya fedha hizo kuwekezwa katika ujenzi wa miundo msingi na uzalisaji.
Aidha kutokana na vita na machafuko ardhi zenye rotuba katika nchi hizo zimeachwa bila kuwepo shughuli za kilimo jambo ambalo limepelekea kupungua mazao ya kilimo.
Kwa mujibu wa takwimu, hali ya tabianchi ijulikanao kama El Nino imezikumba baadhi ya nchi za eneo la maziwa makuu na kusababisha mafuruko au ukame na hivyo kuzidisha umasikini na njaa inayowakumba watu milioni 14 hivi sasa.
Hivi karibuni Shirika la Chakula Duniani WFO lilisema Zambia ambayo iliwahi kuwa mzalishaji mkubwa wa ngano na mahindi hivi sasa inakabiliwa na baa la njaa kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Weledi wa mambo wanasema iwapo vita vitamalizika katika nchi za Afrika na kuwepo mazingira mazuri ya uwekezaji, kwa kuzingatia kuwa nchi hizo zina utajiri asili, basi zinaweza kustawi kiuchumi kwa kasi kubwa.
Umasikini na njaa hutokana na ukosefu wa ajira na hali mbaya ya kiuchumi na kisiasa.
Hali hiyo ikiandamana na mabadiliko ya tabianchi matatizo ya watu wa Afrika huongezeka maradufu na kupelekea kuibuka uhamiaji, vifo na maradhi.
Kwa mantiki hiyo badala ya malumbano kuhusu mipaka na utawala, kuundwa jumuiya za kiuchumi na kuimarishwa uhusiano wa kisiasa na kiuchumi, ni jambo linaloweza kuboresha maisha ya wakaazi wa eneo la Maziwa Makuu Afrika.