Kuondoka askari wa kulinda amani wa Kenya huko Sudan Kusini
Katika hali ambayo, vita na mapigano yanaendelea kushuhudiwa katika nchi ya Sudan Kusini, suala la kuondoka nchini humo baadhi ya askari wa kusimamani amani limegeuka na kuwa changamoto nyingine inayoikabili nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Jumatano ya jana serikali ya Kenya ilianza kuondoa sakri wake huko Sudan Kusini ikiwa ni radiamali yake ya kuachishwa kazi kamanda wake wa kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa Sudan Kusini UNMISS Luteni Jenerali Johnson Mogoa Kimani Ondieki.
Viongozi wa Kenya wametangaza kuwa, kikundi cha kikosi cha askari 100 waliokuwa wakihudumu katika kikosi cha UNMISS Sudan Kusini jana kiliwasili katika uwanja wa ndege wa Nairobi na kwamba, askari wengine wa nchi hiyo watarejea nchini humo kutoka Sudan Kusini katika siku za hivi karibuni. Hatua hiyo imechukuliwa ili kutekeleza amri ya Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo aliyetaka kuondoka askari wa Kenya walioko huko Sudan Kusini.
Shantal Persaud Kaimu Msemaji wa kikosi cha kusimamai amani cha Umoja wa Mataifa Sudan Kusini amesisitiza kuwa, serikali ya Kenya imeanza mpango wa kuwaondoa askari wake kutoka katika mji wa Wau ulioko kaskazini magharibi mwa Sudan Kusini.
Hapana shaka kuwa, uamuzi huo wa serikali ya Kenya umechukuliwa kufuatia hatua ya Umoja wa Mataifa ya kumfuta kazi kamanda Mkenya wa kikosi cha UNMISS, hatua ambayo iliikasirisha serikali ya Nairobi. Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alimfuta kazi Luteni Kanali Johnson Ondieki baada ya ripoti ya uchunguzi kuonyesha kuwa kikosi alichokuwa akikiongoza hakikuwajibika ipasavyo kuwalinda raia wakati mapigano yalipozuka upya nchini Sudan Kusini mwezi Julai mwaka huu.
Ripoti hiyo ilisema, walinda amani waliokuwa chini ya jenerali huyo wa Kenya hawakuchukua hatua yoyote ya kuwalinda raia wakati wanajeshi wa serikali waliposhambulia kituo cha utoaji misaada mjini Juba. Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Kenya iliukosoa vikali uamuzi huo wa Umoja wa Mataifa na kueleza kuwa, hatua hiyo ilichukuliwa pasina ya kushauriana na serikali ya Nairobi.
Kenya inachukua uamuzi wa kuondoa askari wake waliokuwa wakihudumu katika kikosi cha kusimamani amani cha Umoja wa Mataifa huko Sudan Kusini katika hali ambayo, vita na mapigano katika nchi hiyo yangali yanaendelea kushuhudiwa. Kuongezeka mashambulio katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo na vile vile kuuawa raia sambamba na kutekwa nyara vijana wadogo ni mambo yanayoonyesha kwamba, vurugu na machafuko yamechukua mkondo mpya nchini humo.
Baada ya kutiwa saini mkataba wa amani kati ya Rais Salva Kiir na hasimu wake Riek Machar, ilitarajiwa kuwa, hali ya amani na utulivu vingerejea tena huko Sudan Kusini; lakini baada ya kushadidi mapigano na Riek Machar kuikimbia nchi huku akitangaza kwamba, mkataba huo wa amani ni batili, hali ya nchi hiyo kwa mara nyingine tena ilivurugika na machafuko yakaligubika tena taifa hilo.
Machafuko yanaripotiwa kushadidi huko Sudan Kusini katika hali ambayo, kikosi cha kusimamia amani cha UNMISS kinaandamwa na ukosoaji mkubwa. Licha ya kuweko zaidi ya askari elfu 13 wa kusimamia amani huko Sudan Kusini, lakini askari hao wameshindwa kuwalinda raia mkabala na mashambulio dhidi yao. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kukosekana uongozi mzuri wa kikosi hicho ndiyo sababu ya kikosi hicho kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kuwalinda raia kama inavyotakiwa.
Mgogoro wa kisiasa nchini Sudan Kusini unaendelea katika hali ambayo, mbali na kushuhudiwa hali mbaya katika kambi za wakimbizi, akthari ya wananchi wa nchi hiyo wanahitajia misaada ya chakula na dawa. Aidha mlipuko wa ugonjwa wa malaria umepelekea maelfu ya wananchi wa nchi hiyo kukumbwa na maradhi hayo.
Hapana shaka kuwa, kuondoka baadhi ya askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Sudan ni pigo jingine kwa juhudi za kurejesha amani na usalama katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo na inaonekana kuwa, maafisa wa Umoja wa Mataifa wanapaswa kuchukua hatua za haraka za kupeleka askari wengine watakaoziba pengo la askari wa Kenya wanaoondoka.