Jeshi la Misri lawekwa tayari kukabiliana na maandamano ya wananchi
(last modified Fri, 11 Nov 2016 15:04:27 GMT )
Nov 11, 2016 15:04 UTC
  • Jeshi la Misri lawekwa tayari kukabiliana na maandamano ya wananchi

Askari usalama wa Misri wamewekwa katika hali ya tahadhari kwa ajili ya kukabiliana na maandamano ya wananchi yaliyokuwa yamepangwa kufanyika leo kote nchini humo.

Ripoti zinasema kuwa, idadi kubwa ya askari usalama na wajeshi wa Misri walionekana katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kwa shabaha ya kukabiliana na maandamano ya wananchi dhidi ya serikali ya Rais Abdul Fattah al Sisi.

Tangu siku kadhaa zilizopita wanaharakati wa Misri walianzisha kampeni kubwa katika mitandao ya kijamii wakitoa wito wa kushiriki kwa wingi wananchi katika maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika leo kwa jila la 'Mapinduzi ya Watu Maskini'. Sababu kuu ya wito huo ni kulalamikia hali mbaya ya kiuchumi na kijamii nchini Misri.

Maandamano ya wananchi Misri

Baada ya kushika madaraka ya nchi Jenerali Abdul Fattah al Sisi alifanya jitihada za kurejesha utulivu nchini Misri kupitia utekelezaji wa siasa za mkono wa chuma na sera za kipolisi. Hata hivyo viongozi wa serikali ya Cairo wameghafilika kuwa matatizo ya kijamii hayawezi kutatuliwa kwa kutumia ngumi ya chuma na sera za kipolisi. Masuala yanayohusiana na maisha ya watu kama umaskini, ukosefu wa ajira, mfumuko wa bei na kupanda kwa gharama za maisha ni masuala ya kiuchumi lakini yenye taathira kubwa sana katika masuala ya kijamii. Umaskini, ukosefu wa ajira na kupanda kwa gharama za maisha husababisha mparaganyiko wa kijamii na kufuatiwa na malalamiko na maandamano ya wananchi dhidi ya serikali.

Misri katika kipindi cha utawala wa Jenerali al Sisi inasumbuliwa na hali kama hiyo. Kwa kutambua changamoto hiyo ya masuala ya kiuchumi, Jenerali Abdul Fattah al Sisi aliamua kupasisha sheria kali za kutaka kudhibiti malalamiko na upinzani wa wananchi kama ile ya kupambana na ugaidi. Hapana shaka kuwa, moja kati ya matokeo mabaya ya kutumia sera za kipolisi kwa ajili ya kukabiliana na masuala ya kijamii ni kudhoofishwa usalama wa taifa, kwa sababu wakati huo anga ya hofu na vitisho hutawala jamii.

Kamatakamata ya jeshi dhidi ya raia, Misri

Kwa vyovyote vile wito wa kufanya maandamano kulalamikia hali mbaya ya kiuchumi nchini Misri umeungwa mkono na vyama na makundi mbalimbali ya kisiasa. Pamoja na hayo serikali ya Cairo imetumbukia katika makosa yaleyale ya kutumia ngumi ya chuma dhidi ya wananchi, suala ambalo linadhihirisha woga na wahka mkubwa wa watawala wa Misri.

Katika kudumisha sera hizo za ngumi ya chuma, afisa mmoja wa Wizara ya Wakfu ya Misri ametangaza kuwa misikiti ya mikoa yote 27 ya nchi hiyo imefungwa leo baada tu ya Swala ya Ijumaa kutokana na amri ya Waziri wa Wakfu!

Tarehe 7 Novemba Rais Abdul Fattah al Sisi pia aliwataka makamanda na maafisa wa jeshi, polisi na vyombo vya upelelezi kuwa macho kikamilifu.

Abdul Fattah al Sisi

Wachambuzi wa mambo wanasema, serikali ya sasa ya Cairo inafuata nyayo za dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Husni Mubarak za kutumia ngumi ya chuma dhidi ya wananchi wanaodai haki zao za kijamii na kwamba Abdul Fattah al Sisi hajawaidhika wala kupata ibra ya hatima ya madikteta na mafirauni waliomtangulia nchini Misri.  

Tags