Misri yalaani matamshi ya Erdogan kuhusu al Sisi
(last modified Fri, 11 Nov 2016 15:29:57 GMT )
Nov 11, 2016 15:29 UTC
  • Misri yalaani matamshi ya Erdogan kuhusu al Sisi

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imelaani matamshi yaliyotolewa na Rais wa Uturuki kuhusiana na Rais Abdul Fattah al Sisi wa Misri na kuyataja kuwa ni mwendelezo wa hatua za kindumakuwili za serikali ya Ankara.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri, Ahmad Abu Zaidi amelaani matamshi yaliyotolewa na Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki ya kumtaja Rais wa Misri kuwa ni kiongozi asiyewajibika.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri amesema matamshi hayo ya Rais wa Uturuki dhidi ya Rais Abdul Fattah al Sisi ni mwendelezo wa hatua zile zile zisizo na mwelekeo na za kindumakuwili za siasa za Uturuki katika miaka kadhaa ya hivi karibuni.

Rais Erdogan wa Uturuki (kushoto)  na mwenzake wa Misri, al Sisi 

Ahmad Abu Zaid amesema anashangazwa na kusikitishwa  na namna Rais wa Uturuki mwenyewe anavyojiita kuwa ni mlinzi wa demokrasia na uhuru.

Sambamba na kukosoa matamshi ya Rais huyo wa Uturuki, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri amesisitiza kuwa, serikali ya Ankara imewatia mbaroni mamia ya wahadhiri wa vyuo vikuu, wadau wa vyombo vya habari pamoja na makumdi ya wabunge wa nchi hiyo. Amesema serikali ya Uturuki imeyafungia pia makumi ya magazeti na kuwafukuza kazi makumi ya maelfu ya wafanyakazi wa serikali, maafisa wa jeshi na wa vyombo vya mahakama kwa kisingizio cha kuhusika katika jaribio la mapinduzi  nchini humo.

Amesema ni bora Rais Erdogan azingatie ukandamizaji wa kisiasa unaofanyika huko Uturuki badala ya kuingilia masuala ya nchi nyingine.

Tags