AU na EU zatofautiana kuhusiana na ulipaji mishahara ya askari wa AMISOM
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i19375-au_na_eu_zatofautiana_kuhusiana_na_ulipaji_mishahara_ya_askari_wa_amisom
Umoja wa Afrika umekosoa vikali uamuzi wa Umoja wa Ulaya wa kuwalipa mishahara askari wa Burundi wanaohudumu katika kikosi cha kusimamia amani cha AU nchini Somalia AMISOM.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 13, 2016 04:51 UTC
  •  AU na EU zatofautiana kuhusiana na ulipaji mishahara ya askari wa AMISOM

Umoja wa Afrika umekosoa vikali uamuzi wa Umoja wa Ulaya wa kuwalipa mishahara askari wa Burundi wanaohudumu katika kikosi cha kusimamia amani cha AU nchini Somalia AMISOM.

Taarifa ya Umoja wa Afrika imeeleza kuwa, hatua hiyo ya Umoja wa Ulaya ya kuwalipa mishahara askari wa Burundi tu ni ya kibaguzi na kutangaza kuwa, askari hao wa Burundi wako nchini Somalia chini ya usimamizi wa Umoja wa Afrika.

Imeelezwa kuwa, Umoja wa Ulaya umechukua hatua hiyo ya kuwalipa moja kwa moja mishahara askari wa Burundi walioko Somalia ili fedha hizo zisipitie mikononi mwa serikali ya Bujumbura.

Kikosi cha AMISOM kina askari zaidi ya 20,000 wanaoisaidia serikali dhaifu ya Somalia kukabiliana na kundi la kigaidi la Al Shabab. Kikosi hicho cha AMISOM kinajumuisha askari kutoka Uganda, Ethiopia, Burundi, Djibouti, Kenya, na Sierra Leone.

Askari wa AMISOM nchini Somalia

Burundi inashika nafasi ya pili baada ya Uganda kwa kuwa na askari wengi huko nchini Somalia.

Nchi ya Somalia iliyoko katika Pembe ya Afrika imekuwa ikikabiliwa na machafuko kwa miaka kadhaa sasa huku kundi la wanamgambo wa al-Shabab likitishia pakubwa usalama wa nchi hiyo na hata wa nchi jirani.

Mbali na ukosefu wa usalama, Somalia imekuwa ikikabiliwa na tatizo kubwa la ukame na baa la njaa hali ambayo imewafanya baadhi ya raia kuikimbia nchi hiyo na kuomba hifadhi katika nchi jirani hususan Kenya.