UN: Raia hawana makaazi na mapigano yanaendelea Galkayo, Somalia
Karibu watu 90,000 katika mji wa Galkayo nchini Somalia wameendelea kubaki bila makaazi kutokana na kuzidi hali ya wasiwasi na mapigano ya mara kwa mara baina ya vikosi vya maeneo yanayojiendeshea masuala yao ya ndani ya Galmudug na Puntland.
Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ambayo imeeleza kuwa watu wapatao 40,000 kati ya hao wamepoteza tena makazi ya dharura waliyokuwa wamepatiwa.
Mapigano katika mji wa Galkayo ulioko eneo la kaskazini-kati mwa Somalia yameendelea kushuhudiwa licha ya makubaliano ya usitishaji vita yaliyosainiwa tarehe mosi ya mwezi huu wa Novemba mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu baina ya viongozi wa maeneo ya Galmudug na Puntland.
Kwa mujibu wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Idadi ya Watu (UNFPA), eneo la Galkayo lina watu wapatao 270,000.
Baada ya makubaliano ya Abu Dhabi, pande mbili za Galmudug na Puntland zilikutana tena katika duru nyingine ya mazungumzo ya amani yaliyofanyika hivi karibuni huko Bosasso ambapo ulitolewa wito wa kuzitaka zitekeleze makubaliano ya kusitisha mapigano.
Huku mgogoro wa Galkayo ukiwa unaendelea kuvuruga hali ya maisha ya watu waliokuwa tayari wameshapoteza makazi yao, ripoti za Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu zimeeleza kuwa akthari ya watu waliopoteza makaazi yao wamekuwa wakikimbilia vijiji vya mbali ili kuweza kuendelea kuishi.
Maafisa wa afya wanakadiria kuwa watu 45 wameuawa na wengine 162 wamejeruhiwa tangu Oktoba 7 mwaka huu. Mapigano yanayoendelea katika eneo la Galkayo yamevuruga pia shughuli za masomo za wanafunzi wapatao 20,000 kwa wiki ya tano mtawalia.../