Sera za kujipanua za Saudia dhidi ya maslahi ya Misri
Ripoti za vyombo vya habari zinaeleza kuwa Utawala wa Aal Saud umezusha madai mapya ya umiliki wa ardhi za Misri na kuanzisha propaganda za kupotosha ukweli wa historia kwa ajili ya kufanikisha tamaa zake za kujipanua.
Kuhusiana na suala hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Adel al-Jubeir amedai kwamba kuna nyaraka za tangu zama za utawala wa Othmaniyah zinazothibitisha kuwa visiwa vya Misri vya Tiran na Sanafir ni milki ya utawala wa Riyadh.
Hii ni katika hali ambayo Hamdin Sabahi aliyekuwa mgombea katika uchaguzi wa rais wa Misri na mwasisi wa harakati ya wananchi hapo kabla alitoa matamshi yanayokinzana na madai ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia akisisitiza kwamba kutokana na makubaliano ya Oktoba mosi mwaka 1906 ambayo yalisainiwa kati ya dola la Othmaniyah na Misri, visiwa vya Tiran na Sanafir ni sehemu isiyotenganishika na ardhi yote ya Misri.
Sisitizo la Saudia la kudai kuwa na umiliki katika sehemu ya ardhi ya Misri linatolewa katika hali ambayo hivi karibuni Mahakama ya Misri ilitoa hukumu ya kuthibisha kuwa visiwa vya Tiran na Sanafir ni milki ya nchi hiyo. Mahakama ya rufaa ya kiidara ya Misri ilitupilia mbali rufaa ya serikali ya nchi hiyo ya kupinga uamuzi wa awali wa mahakama hiyo wa kubatilisha makubaliano ya kuainisha mipaka ya baharini yaliyosainiwa kati ya Misri na Saudia ambayo yaliupatia utawala wa Riyadh haki ya umiliki wa visiwa viwili vya Tiran na Sanafir.
Itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Aprili mwaka huu Mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudi Arabia alifanya safari iliyogubikwa na vituko vingi nchini Misri. Katika safari hiyo Cairo na Riyadh zilisaini makubaliano ambayo yaliipatia Saudia umiliki wa visiwa viwili vya Tiran na Sanafir. Hatua hiyo iliyochukuliwa na Rais Abdel Fattah el Sisi kupitia mkataba wa kuainisha mipaka ya baharini baina ya Misri na Saudia ilikabiliwa na upinzani na malalamiko makubwa ndani ya Misri.
Wapinzani wa uamuzi wa El Sisi waliandaa maandamano kadhaa ya kupinga uamuzi huo lakini serikali ya jenerali huyo wa zamani wa jeshi iliyachukulia maandamano hayo kama kihatarishi cha usalama na kuwatia mbaroni mamia ya waandamanaji mbali na idadi kadhaa miongoni mwao waliopigwa risasi wakauawa na kujeruhiwa.
Malalamiko ya upinzani yamesambaa hadi nje ya jamii ya kiraia ya Misri. Kwa mujibu wa baadhi ya duru za habari utendaji wa Rais Abdel Fattah el Sisi hususan hatua yake ya kuuza ardhi ya Misri umepingwa na kulalamikiwa hata ndani ya jeshi la nchi hiyo. Katika kuendeleza ukandamizaji dhidi ya wanaompinga, Rais wa Misri ametoa amri ya kutiwa nguvuni na kuwekwa kizuizini maafisa kadhaa wa ngazi za juu wa jeshi kwa kisingizio cha kuhusika na njama ya kufanya mapinduzi ya kijeshi. Hali ya kuwa inavyoonekana sababu kuu ya malalamiko ya umma ni hatua ya Abdel Fattah el Sisi ya kuutunukia utawala wa Aal Saud visiwa viwili vya Misri vya Tiran na Sanafir. Hatua ya serikali ya Cairo imegeuka kuwa mgogoro mwingine mpya wa kiusalama ndani ya Misri. Wamisri wamekasirishwa na kuulaani utawala wa Cairo baada ya kuelewa kwamba visiwa ambavyo ni milki ya nchi yao vimetolewa na Jenerali El Sisi kama moja ya bakhshishi makhsusi kwa Saudia. Wananchi na wanaharakati wa kisiasa nchini Misri wanaamini kuwa utawala wa Aal Saud umelitumia vibaya suala la visiwa vya Misri kutokana na kuelewa shida kubwa ya fedha iliyonayo serikali ya Cairo.
Wananchi wengi wa Misri wanaitakidi kuwa makubaliano ya karibuni kati ya nchi yao na Saudia wakati wa safari ya Mfalme Salman nchini Misri na propaganda nyingi zilizofanywa na pande mbili kuhusiana na safari hiyo, na vilevile makubaliano kadhaa yaliyofikiwa baina ya pande mbili katika safari hiyo hususan ya kuipatia serikali ya Riyadh umiliki wa visiwa viwili, kwa namna fulani yanalenga kudhoofisha nafasi ya kieneo ya Misri na kuridhiwa udhoofishaji huo na seriali ya El Sisi.
Makubaliano hayo yanakiuka kifungu cha 151 cha Katiba ya Misri kinachoeleza bayana kwamba mikataba na makubaliano yote yanayohusu mamlaka ya kujitawala lazima yaidhinishwe kupitia kura ya maoni.
Inavyoonyesha, matukio ya karibuni yameifanya serikali ya Misri nayo pia iangalie upya siasa zake kuhusina na Saudi Arabia; na mabadiliko hayo katika msimamo wa Cairo yamewakasirisha viongozi wa Aal Saudi; na madai mapya kuhusiana na umiliki wa ardhi yaliyotolewa na Riyadh lengo lake ni kutaka kuwatia shemere tena viongozi wa Misri ili watii na kutekeleza madai hayo mapya ya Saudia…/