Jeshi la Nigeria laanzisha operesheni kali dhidi ya Boko Haram
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1972-jeshi_la_nigeria_laanzisha_operesheni_kali_dhidi_ya_boko_haram
Jeshi la Nigeria limeanzisha operesheni kali dhidi ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram, ambayo ina lengo la kuwasambaratisha wanachama wa kundi hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 26, 2016 04:18 UTC
  • Jeshi la Nigeria laanzisha operesheni kali dhidi ya Boko Haram

Jeshi la Nigeria limeanzisha operesheni kali dhidi ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram, ambayo ina lengo la kuwasambaratisha wanachama wa kundi hilo.

Mkuu wa Jeshi la Nigeria, Luteni Jenerali Tukur Buratai amesema hayo katika mkutano wake na viongozi wa makabila katika mji wa Maiduguri ambayo ni makao makuu ya jimbo la Borno lililoko kaskazini mashariki mwa Nigeria na kusisitiza kwamba, jeshi la nchi hiyo limeingia katika operesheni ya kusafisha maeneo ya mbalimbali na uwepo wa wanamgambo wa Boko Haram. Amesema matunda ya operesheni hiyo ni kurahisisha kukombolewa raia wanaoshikiliwa na kundi hilo wakiwemo wanafunzi wa mji wa Chibok ulioko katika jimbo la Borno.

Mkuu wa majeshi ya Nigeria amesema kwa sasa jeshi la nchi hiyo limepewa majukumu matatu. Amesema, jukumu la kwanza ni kuendesha mapambano dhidi ya Boko Haram, pili kuwakomboa mateka wanaoshikiliwa na wanachama wa kundi hilo na jukumu la tatu ni kuendesha operesheni ya kijeshi kaskazini mashariki mwa Nigeria kwa shabaha ya kurejesha amani na utulivu katika maeneo hayo.

Takwimu zinaonyesha kuwa, watu zaidi ya 20,000 wameuawa na wengine zaidi ya milioni 2.5 wamelazimika kuwa wakimbizi katika nchi yao, tangu kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram lianzishe hujuma zake nchini Nigeria mwaka 2009.