Kukandamizwa waandishi wa habari nchini Misri
Habari kutoka nchini Misi zinaonesha kuendelea kukandamizwa waandishi wa habari na serikali ya Rais Abdul Fattah el Sisi wa nchi hiyo na kuzidi kubanwa tasnia ya uandishi wa habari katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Hatua ya karibuni kabisa ni kitendo cha mahakama moja ya Misri cha kuwafunga jela miaka miwili mkuu wa chama cha waandishi wa habari na wanachama wawili wa chama hicho.
Mahakama hiyo imedai kuwa, miezi sita iliyopita, Yahiya Kallash, mkuu wa chama cha waandishi wa habari cha Misri pamoja na Gamal Abd el-Rahim, Katibu Mkuu wa chama hicho na Khaled Elbalshy, mkuu wa kamati ya uhuru wa vyama, waliwaficha waandishi wawili wa habari waliokuwa wanatafutwa na serikali.
Viongozi hao waandamizi wa chama cha waandishi wa habari cha Misri walitiwa mbaroni miezi sita iliyopita baada ya polisi kuvamia jengo la chama hicho kwa lengo la kuwakamata waandishi waliokuwa wanatafutwa na serikali.
Yahiya Kallash alikilalamikia vikali kitendo cha polisi cha kuwatia mbaroni Amr Badr na Mahmoud El Sakka, waandishi wa habari waliokuwa wanaikosoa serikali na kusema kuwa, serikali ya Misri imeanzisha vita dhidi ya uandishi na waandishi wa habari nchini Misri.
Waandishi Amr Badr na Mahmoud El Sakka wanatumuhimuwa kuandaa maandamano ya kulalamikia kitendo cha serikali ya Cairo cha kuipa Saudi Arabia visiwa viwili vya Misri vya Tiran na Sanafir.
Katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, serikali ya Rais Abdul Fattah el Sisi imeongeza mashinikizo yake dhidi ya waandishi wa habari na wanaharakati wa kisaisa na kupelekea kuzidi kutanda hali ya wasiwasi katika jamii ya nchi hiyo.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, lengo la viongozi wa Misri la kushadidisha mashinikizo dhidi ya wanaharakati wja kisiasa ni kujaribu kuzima sauti ya uhuru na ukombozi ya wananchi wa Misri. Wapinzani wa serikali ya Cairo wanaendelea kukandamizwa katika hali ambayo serikali ya Rais el Sisi imeweka sheria ya kupambana na ugaidi kwa lengo la kupata fursa ya kuwakandamiza zaidi wapinzani wa kisiasa wa serikali hiyo.
Kwa mujibu wa sheria hiyo ya ugaidi, serikali ya Misri ina uwezo wa kukandamiza mkusanyiko wowote ule na kukandamiza upinzani wa aina yoyote ile kwa madai ya kupambana na ugaidi.
Waandishi wa habari wa ndani na nje ya Misri wanalalamika kuwa sheria hiyo ya ugaidi inakwamisha shughuli za uwandishi wa habari na kufikisha kwa walimwengu kilio cha wananchi wa Misri. Sheria ya kupambana na ugaidi ya nchini Misri ina vifungu vitano ambapo moja ya kifungu chake kinasema, waandishi wa habari hawana haki ya kufichua taarifa yoyote ile ambayo inakinzana na taarifa iliyotolewa na serikali.
Wanaharakati wa kisiasa nchini Misri wanaendelea kuilalamikia vikali sheria hiyo kandamizi na wanasema kuwa, lengo la kupasishwa sheria hiyo si kupambana na ugaidi bali ni kuzuia ustawi wa demokrasia nchini humo. Kwa mtazamo wa wananchi wa Misri, nchi hiyo hivi sasa haina tofauti yoyote na kipindi cha urais wa Hosni Mubarak, dikteta aliyepinduliwa na wananchi nchini humo.
Wakati wa utawala wa dikteta Hosni Mubarak, Misri iliishi katika hali ya hatari kwa muda wa miaka 30. Wakati huo hakuna mtu yeyote aliyeruhusiwa kunyanyua mdomo wake kuikosoa serikali kwani kuliwekwa sheria kali sana dhidi ya jambo hilo. Hivi sasa pia hali imeendelea kuwa hiyo hiyo licha ya kutangazwa kwa mdomo kuwa sheria ya hali ya hatari imeondolewa. Hivi sasa pia mtu yeyote anayeikosoa serikali anakumbwa na adhabu kali na kila leo watu wanatiwa mbaroni na kufungwa jela kwa makosa ya kufanya maandamano ya kuilalamikia serikali. Si hayo tu, lakini waandishi wa habari nao wanalengwa moja kwa moja na sheria mbalimbali zilizowekwa na serikali, za kubana uandishi na waandishi wa habari.
Ukandamizaji huo mkubwa unafanyika katika hali ambayo, baada ya Abdul Fattah el Sisi kuongoza jeshi kumpindua Rais wa kwanza kuchaguliwa na wananchi wa Misri, Muhammad Morsi, alisema kuwa lengo lake ni kusimamia demokrasia na kuhakikisha kuwa Misri inafuata mkondo sahihi wa kidemokrasia. Lakini hakuna chochote kilichoshuhudiwa kutoka kwake ghairi ya kuzidi kuwakandamiza wanaharakati wa kisiasa na kuunda serikali ya kipolisi inayoendeshwa na majenerali wa kijeshi nchini humo.