Wanafunzi wateketeza kwa moto chuo kikuu Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1993-wanafunzi_wateketeza_kwa_moto_chuo_kikuu_afrika_kusini
Wanafunzi waliogoma nchini Afrika Kusini wameteketeza kwa moto majengo kadhaa ya chuo kikuu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 26, 2016 12:47 UTC
  • Wanafunzi wateketeza kwa moto chuo kikuu Afrika Kusini

Wanafunzi waliogoma nchini Afrika Kusini wameteketeza kwa moto majengo kadhaa ya chuo kikuu.

Imearifiwa kuwa wanafunzi waliokuwa na hasira wa Chuo Kikuu cha North West wameteketeza kwa moto jengo la idara na kituo cha sayansi chuoni hapo katika mji wa Mahikeng, ambao pia unajulikana kama Mafikeng. Kufuatia tukio hilo la Jumatano usiku, wanafunzi wote wametakiwa kuondoka chuoni hapo mara moja.

Machafuko hayo yaliibuka wakati wa uzinduzi wa baraza jipya la wanachuo wakati baadhi ya wanafunzi walipovuruga shughuli hiyo na kisha kushambuliwa na maafisa wa usalama waliojaribu kuwatawanya.

Baraza lililopita la wanafunzi chuoni hapo lilitaka lugha ya Kiafrikaans ya makaburu iondolewe kama lugha ya kufundishia na kusema utumizi wa lugha hiyo unawafaidisha wanafunzi wazungu tu.

Katika siku za hivi karibuni kumeibuka machafuko baina ya wanafunzi wazalendo waafrika na wazungu kuhusu utumizi wa Kiafrikaans, lugha ambayo inatazamwa na wazalendo wengi kama lugha ya wazungu madhalimu wakati wa mfumo wa ubaguzi wa rangi au Apertheid kuanzia muongo wa 40 hadi muongo wa 90.

Mara kwa mara Afrika Kusini hushuhudia migomo ya wanafunzi ambao hulalamikia mambo kadhaa kama vile ukosefu wa mabweni, ada ya juu na kuendelea kuwepo mabaki ya zama za ubaguzi wa rangi vyuoni.