Afisa wa polisi Somalia auawa katika mripuko wa bomu
Afisa mmoja wa ngazi ya juu nchini Somalia ameuawa katika hujuma iliyofanywa na magaidi wanaosaidikiwa kuwa ni wanachama wa ash-Shabab.
Abdifitah Omar Halane, Msemaji wa gavana wa Mogadishu, mji mkuu wa Somalia amesema kuwa, afisa huyo wa polisi ameuawa jioni ya jana katika shambulizi la bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari katika barabara yenye msongamano wa watu ya eneo la Shibis, mjini Mogadishu. Kwa mujibu wa Halane, askari wengine watatu waliokuwa eneo la tukio wamejeruhiwa. Ameongeza kuwa, polisi imeanzisha uchunguzi kwa lengo la kuwabaini wahusika wa jinai hiyo.
Hadi sasa hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na shambulizi hilo, ingawa kidole cha lawama kimeelekezwa kwa wanachama wa kundi la kigaidi la ash-Shabab ambalo ni maarufu kwa kufanya jinai hizo. Shambulizi hilo limetokea katika hali ambayo polisi ya Somalia kwa kushirikiana na askari wa Kusimamia amani wa Umoja wa Afrika (AMISOM) wameimarisha usalama kutokana na kukaribia tarehe ya uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika tarehe 30 ya mwezi huu.