UN: Waniger milioni mbili wanahitaji misaada ya kibinadamu
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu wapatao milioni mbili watahitaji misaada ya kibinadamu nchini Niger.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imetoa ripoti katika mji mkuu wa Niger, Niamey na kutangaza kuwa hali mbaya ya kibinadamu katika nchi hiyo imesababishwa na kukosekana usalama wa chakula, utapiamlo, maradhi ya kuambukiza, mafuriko na raia kupoteza makazi yao kutokana na mgogoro wa ndani.
Makadirio yaliyofanywa na asasi hiyo ya Umoja wa Mataifa yanaonyesha kuwa mnamo mwaka 2017 karibu watu milioni mbili; laki tatu na elfu 40 kati yao wakiwa wakaazi wa eneo la Diffa lililoko kusini mashariki mwa Niger watahitaji misaada ya kibinadamu.
Ripoti hiyo ya OCHA imefafanua kuwa nusu ya watu milioni moja na laki tatu wanaohitaji misaada hiyo ya kibinadamu ni wanawake ambao wanakabiliwa na hali mbaya mno ya lishe duni.
Katika miaka ya karibuni, nchi ya Niger ambayo iko magharibi mwa Afrika imekuwa ikikabiliwa kila mara na tatizo la hali mbaya ya uhaba wa chakula.
Hii ni pamoja na kwamba tangu mwaka uliopita wa 2015 kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram la nchini Nigeria nalo pia limekuwa tishio kwa amani na uthabiti wa Niger.../