Watu 30 wauawa katika hujuma ya kigaidi Mogadishu, Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i20239-watu_30_wauawa_katika_hujuma_ya_kigaidi_mogadishu_somalia
Watu wasiopungua 30 wamepoteza maisha katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu kufuatia hujuma mbaya zaidi dhidi ya raia kuwahi kushuhudiwa mjini humo katika miaka ya hivi karibuni.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Nov 26, 2016 12:23 UTC
  • Watu 30 wauawa katika hujuma ya kigaidi Mogadishu, Somalia

Watu wasiopungua 30 wamepoteza maisha katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu kufuatia hujuma mbaya zaidi dhidi ya raia kuwahi kushuhudiwa mjini humo katika miaka ya hivi karibuni.

Taarifa zinasema muda wa saa sita mchana hivi, gaidi aliyekuwa akiendesha gari lililosheheni bomu aliliripua katika soko wazi la mboga na matunda katika mtaa wa Afesyoni ulio wilayani Waberi mjini Mogadishu. Bomu hilo linasadikiwa kuwa lilikuwa linalenga kituo cha polisi karibu na Chuo cha Sayansi na Teknolojia mjini Mogadishu kilichokuwa kikitembelewa na Rais Hassan Sheikh Mahmoud wakati wa hujuma hiyo ya kigaidi.

Shambulizi hilo limefanyika katika lango la kuingia soko la Beerta ambalo liko karibu mji Uwanja wa Ndege wa Mogadishu. Moshi umeonekana ukiwa umetanda kote katika mtaa huo.

Hakuna yeyote aliyedai kuhusika na hujuma hiyo lakini inashabihiana na hujuma ambazo hutekelezwa na kundi la kigaidi la Al Shabab linalofungamana na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda.

Shambulizi hilo limetokea katika hali ambayo polisi ya Somalia kwa kushirikiana na askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika (AMISOM) wameimarisha usalama kutokana na kukaribia tarehe ya uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika tarehe 30 ya mwezi huu.