El Sisi: Misri si mtumwa wa Saudi Arabia
-
Rais Abdul Fattah el Sisi wa Misri
Rais wa Misri amesema, nchi yake kamwe haiwezi kufuata maamrisho ya Saudi Arabia katika mahusiano yake ya kieneo na kimataifa.
Gazeti la al Safir la nchini Lebanon limemnukuu Rais Abdul Fattah el Sisi akisema hayo mjini Cairo na kuongeza kuwa, Misri si mtumwa wa Saudi Arabia katika uhusiano wake wa kieneo na kimataifa.
Gazeti hilo limenukuu duru za kuaminika kutoka Ikulu ya Misri zikithibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, wakati wa mazungumzo yake na Mfalme wa Kuwait, Amir Sabbah Ahmad Jabir al Sabbah yaliyohusu umilikaji wa visiwa viwili vinavyogombaniwa baina ya Saudia na Misri, Rais Abdul Fattah el Sisi amesema, amechoshwa na mashinikizo wanayowekewa viongozi wa Misri, na kutaka kukomeshwa mara moja mashinikizo hayo.
Aidha Rais wa Misri amesema, Saudi Arabia inapaswa kuziheshimu nchi nyingine zenye misimamo ya kisiasa tofauti na yake katika masuala ya kieneo na kimataifa na itambue kuwa Misri si nchi ndogo ya kuweza kuburuzwa na Saudia.
Ugomvi baina ya Misri na Saudi Arabia ulizidi kuwa mkubwa baada ya Misri kuunga mkono muswada uliowasilishwa na Russia kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na Syria.