Kuanza oparesheni ya kuwaaangamiza wanamgambo wa Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i2044-kuanza_oparesheni_ya_kuwaaangamiza_wanamgambo_wa_boko_haram_kaskazini_mashariki_mwa_nigeria
Jeshi la Nigeria limesema kuwa tayari limeanza oparesheni ya kuwaangamiza wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika majimbo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 27, 2016 09:32 UTC
  • Kuanza oparesheni ya kuwaaangamiza wanamgambo wa Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria

Jeshi la Nigeria limesema kuwa tayari limeanza oparesheni ya kuwaangamiza wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika majimbo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Jenerali Tukur Buratai mmoja wa makamanda wa jeshi la Nigeria amesisitiza katika kikao na wakuu wa kikabila wa mji wa Maiduguri makao makuu ya jimbo la Borno huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo kwamba vikosi vya Nigeria tayari vimeanzisha oparesheni ya kuwaangamiza wanamgambo wa kundi la Boko Haram katika jimbo la Borno.

Jenerali Buratai ameongeza kuwa vikosi vya Nigeria vimepatiwa majukumu matatu. La kwanza likiwa ni kuendesha mapambano dhidi ya Boko Haram ambapo vikosi vya jeshi hilo tayari vimepata mafanikio. Jenerali Tukur Buratai ambaye ni mmoja wa makamanda wa jeshi la Nigeria amekumbusha kuwa marhala ya pili ya kazi waliyopatiwa vikosi hivyo ilikuwa ni kuwakomboa watu waliotekwanyara.

Wanamgambo wa Boko Haram wasiopungua 92 wameuawa na watu 850 ambao walikuwa wakishikiliwa mateka na kundi hilo katika kijiji cha Kumshe nchini Nigeria , wamekombolewa kwenye oparesheni ya pamoja iliyotekelezwa na jeshi la Cameroon na vikosi vya Nigeria, Chad, na Niger dhidi ya ngome za Boko Haram.

Wakati huohuo serikali ya Cameroon pia imesisitiza kufanya oparesheni ya pamoja ya kijeshi na jeshi la Nigeria dhidi ya Boko Haram katika mipaka ya nchi mbili hizo.

Issa Tchiroma Bakary Waziri wa Mawasiliano wa Cameroon amesema silaha na zana za kijeshi zimenaswa katika kambi ya Boko Haram karibu na mipaka ya Cameroon.

Hadi kufikia sasa viongozi wa serikali ya Nigeria bado hawajathibitisha au kukadhibisha habari hiyo. Kundi la Boko Haram katika wiki za hivi karibuni lilizidisha mashambuli ya kigaidi katika vijiji vilivyopo katika majimbo ya kaskazini mwa Cameroon.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na serikali ya Cameroon, mwaka uliopita pekee, raia karibu elfu moja wa kaskazini mwa nchi hiyo waliuawa katika mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram. Taasisi za kutetea haki za binadamu zinaamini kuwa kundi la Boko Haram ni kundi katili zaidi linalobeba silaha duniani.

Kundi la Boko Haram huwaozesha kwa nguvu watoto katika mlolongo wa hujuma na vitendo vyake vya ukatili linalovyovifanya khususan dhidi ya watoto, mbali na kuwadhalilisha kijinsia. Kuwatekanyara wanawake na watoto na kutekeleza mauaji ya kikatili dhidi ya raia, yote hayo yamezipelekea familia zinazoishi katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria kutowapeleka shule watoto wao.

Katika mazingira kama hayo, Afisa mmoja wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe amezungumzia kuhusu mpango wa kutumwa nchini Nigeria washauri maalumu wa kijeshi wa Marekani. Afisa huyo ameongeza kuwa Wizara ya Ulinzi ya Marekani iliishauri serikali ya Rais Barack Obama wa nchi hiyo isaidie kutuma washauri maalumu wa kijeshi wa Pentagon kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa jeshi la Nigeria ili kupambana na Boko Haram.

Huko nyuma Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria aliiomba serikali ya Marekani isaidie kupanua mapambano dhidi ya kundi hilo. Gazeti la New York Times kwa mara ya kwanza pia liliweza kuashiria kuhusu kutuwma washauri maalumu wa kijeshi wa Marekani kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vikosi vya Nigeria.

Gazeti la New York Times pia limeandika habari kuhusu kutumwa nchini Nigeria hapo jana wanashauri wa oparesheni maalumu. Pamoja na hayo yote, maafisa wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani wamekanusha kutumwa washauri wa oparesheni maalumu nchini Nigeria na kusisitiza kuwa pendekezo lililotolewa na serikali ya Washington linaendelea kujadiliwa; na kwamba suala la kutuma washauri wa Marekani huko Nigeria linapasa kuidhinishwa na serikali ya Marekani. Inafaa kuashiria hapa kuwa uhusiano wa nchi mbili hizo uliingia dosari mwishoni mwa mwaka juzi wa 2014. Hatua ya viongozi wa Marekani ya kusema kuwa serikali ya Rais wa wakati huo wa Nigeria Goodluck Jonathan imeshindwa kuwalinda raia wa nchi hiyo dhidi ya mashambulizi ya Boko Haram ilisababisha kuyumba uhusiano kati ya Abuja na Washington. Uhusiano wa Nigeria na Marekani umeboreka sasa tangu Muhammadu Buhari aingine madarakani kufuatia uchaguzi wa Rais wa mwaka jana. Buhari alifanya ziara mjini Wasington mwezi Julai mwaka jana na kulakiwa pakubwa na viongozi wa ikulu ya Marekani (White House).