Zoezi la kuhesabu kura Ghana linaendelea; Rais Mahama anaongoza kwa tofauti ndogo
Zoezi la kuhesabu kura nchini Ghana linaendelea huku taarifa za awali zikionyesha kuwa, mataokeo yasiyo rasmi yanaonyesha kwamba, Rais John Dramani Mahama anaongoza akifuatiwa kwa karibu na kiongozi wa upinzani Nana Akufo-Addo.
Rais John Mahama ambaye aliingia madarakani mwaka 2012 kufuatia kifo cha Rais John Atta Mills anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Nana Akufo-Addo mgombea wa chama cha upinzani cha NNP.
Hata hjivyo Tume ya Uchaguzi ya Ghana imeamua kuchukua tahadhari na kusema kuwa, itatangaza matokeo hayo baada ya zoezi la kuhesabu kura kukamilika. Taarifa ya Tume ya Uchaguzi ya Ghana imewataka wananchi kudumisha utulivu na kusubiri matokeo yatakayotangazwa na tume hiyo.
Wadukuzi wa mitandao jana walivamia mtandao wa Tume ya Uchaguzi nchini Ghana na kuuvuruga siku moja baada ya uchaguzi wa urais katika taifa hilo la magharibi mwa Afrika. Tume ya uchaguzi imelaani vikali kitendo hicho.
Wakati huo huo, Nana Akufo-Addo kiongozi wa upinzani anayechuana katika uchaguzi huo na Rais John Dramani Mahama amesema kuwa, ana uhakika wa kuibuka na ushindi katika uchaguzi huo.
Aidha kiongozi huyo wa upinzani amedai kuwa, chama chake cha NPP kimejinyakulia viti vingi vya Ubunge ikilinganishwa na vya chama tawala.
Viongozi wa upinzani nchini Ghana wameeleza wasiwasi walionao kutokana na kile walichokisema kuwa, kuweko njama za kutaka kuchakachua matokeo ya uchaguzi huo.