Rais mteule Gambia: Jammeh hana mamlaka ya kukataa matokeo ya uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i21184-rais_mteule_gambia_jammeh_hana_mamlaka_ya_kukataa_matokeo_ya_uchaguzi
Rais mteule wa Gambia amesema kuwa, Rais Yahya Jammeh ambaye alishindwa katika uchaguzi wa Rais wa Disemba Mosi, hana mamlaka ya kikatiba ya kukataa matokeo ya uchaguzi huo na wala katiba haimruhusu kuitisha uchaguzi mwingine.
(last modified 2026-05-02T17:46:50+00:00 )
Dec 11, 2016 02:29 UTC
  • Rais mteule Gambia: Jammeh hana mamlaka ya kukataa matokeo ya uchaguzi

Rais mteule wa Gambia amesema kuwa, Rais Yahya Jammeh ambaye alishindwa katika uchaguzi wa Rais wa Disemba Mosi, hana mamlaka ya kikatiba ya kukataa matokeo ya uchaguzi huo na wala katiba haimruhusu kuitisha uchaguzi mwingine.

Adama Barrow ambaye alitangazwa na tume ya uchaguzi wa Gambia kuwa mshindi wa uchaguzi huo wa rais baada ya kupata asilimia 45.5 ya kura amesema kuwa, yuko tayari kufungua mlango wa mazungumzo ili kumkinaisha Jammeh akabidhi madaraka ya nchi kwa amani kwa ajili ya maslahi ya taifa hilo la magharibi mwa Afrika.

Hatua ya Rais Jammeh ya kutangaza kwamba, anapinga matokeo ya uchaguzi huo na kutoa wito wa kufanyika uchaguzi mwingine imewashangaza wengi hasa kwa kutilia maanani kwamba, kiongozi huyo aliyetawala Gambia kwa zaidi ya miaka 20 hapo awali alikiri kushindwa. 

Yahya Jammeh

Hatua ya Jammeh ya kukubali kushindwa hata kabla yakumalizika zoezi la kuhesabu kura, iliwapa matumaini raia walioona kama mwisho wa utawala wa kimabavu wa zaidi ya miongo miwili ulikuwa umemalizika.

Viongozi mbalimbali wametoa wito kwa Rais Jammeh kuyakubali matokeo na kukabidhi madaraka kwa njia ya amani. Ubalozi wa Marekani katika mji mkuu Banjul, umetoa wito kwa wanajeshi kuheshimu matakwa ya wananchi wengi wa Gambia ambao wamemchagua Adama Barrow.

Nchi jirani ya Senegal imetoa mwito kwa Rais Jammeh kukabidhi madaraka kwa mshindi kwa njia ya amani huku wasiwasi ukitanda wa nchi hiyo kutumbukia katika machafuko.

Jana Gambia ilimzuia kuingia nchini humo, Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf ambaye pia ni mwenyekiti wa hivi sasa wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika ECOWAS aliyekusudia kwenda kufanya upatanishi.