Upinzani: Mpango wa mageuzi ya ardhi wa Zimbabwe umeharibu uchumi
Mwanachama wa chama cha upinzani kujulikanacho kwa jina la People’s Democratic (PDP) amedai kuwa serikali ya Rais Robert Mugabe imeharibu kikamilifu uchumi wa nchi hiyo wakati ilipoanzisha mpango wa marekebisho ya ardhi mwaka 2000.
George Mkhwanazi Naibu Msemaji wa chama cha upinzani cha PDP amesema kuwa, inatia wasiwasi kuona serikali ya Zimbabwe inashindwa kuwadhaminia chakula wananchi kutokana na mpango huo wa marekebisho ya ardhi. Mkhwanazi amesema, serikali ya Zimbabwe inayoongozwa na chama cha Zanu-PF iliruhusu suala hilo la marekebisho ya ardhi kuendelea kwa muda mrefu bila ya kupatiwa ufumbuzi, wakati huo Wazimbabwe wakidhani kuwa wangeweza kunufaika katika hali ambayo hakukuwa na mpango wowote wa kuwanufaisha. Hata hivyo Mbunge wa chama tawala Zanu-Pf Joseph Tshuma amepinga madai ya naibu msemaji wa chama cha upinzani cha PDP akisema kuwa msemaji huyo ni muungaji mkono mkubwa wa nchi za kibeberu ambazo zilimuwekea vikwazo Rais Mugabe na watu wake wa karibu kufuatia tuhuma za kuwepo ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu huko Zimbabwe.