Magaidi wa ISIS waua raia 12 Sinai, Misri
Magaidi wanaofungamana na kundi la kigaidi la ISIS au Daesh nchini Misri wameua raia 16 katika Rasi ya Sinai kwa tuhuma za kushirikiana na jeshi la serikali.
Taswira za video zilizosambazwa katika intaneti zinaonyesha magaidi wa kundi la Wilayat Sinai wanaofungamana na ISIS wakiwa wamewaua vijana 16 katika eneo linalokumbwa na msukosuko la Rasi ya Sinai.
Kwa mujibu wa taarifa vijana hao ima walipigwa risasi au kukatwa shingo zao na magaidi wa kundi hilo ambalo zamani likijulikana kama Ansar Bait al Maqdis ambalo mwaka 2014 lilitangaza utiifu kwa kundi la kigaidi la ISIS.
Tangu wakati huo jeshi la Misri limepiga kambi kaskazini mwa nchi hiyo kwa ajili ya kupambana na magaidi hao wakufurishaji ambao wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara ya kigaidi.
Katika kipindi chote hiki cha miaka miwili cha tangu kuanza operesheni za jeshi la Misri kaskazini mwa nchi hiyo, mashambulizi ya makundi yenye silaha sio tu hayajapungua, lakini pia idadi ya raia wanaouawa nayo imeongezeka, huku jeshi la Misri likiwa ni miongoni mwa pande zinazolaumiwa kwa kutokuwa makini katika kupambanua baina ya magaidi na raia wa kawaida kwenye mashambulizi yake.