Rais wa Sudan Kusini ataka kufanyika Mazungumzo ya Kitaifa
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ametoa wito wa kufanyika 'Mazungumzo ya Kitaifa' ili kuupatia ufumbuzi mzozo wa kisiasa na kiusalama unaoikabili nchi hiyo.
Akihutubia bunge hapo jana Jumatano, Rais Kiir alisema mazungumzo tu ndiyo yanayoweza kutatua migawanyiko na mzozo uliopo sambamba na kurejesha amani katika nchi hiyo ya Kiafrika.
Bila kutaja majina ya watakaojumuishwa kwenye jopo la mazungumzo hayo, Rais wa Sudan Kusini amesema shakhsia na watu mashuhuri watatoa miongozo katika mazungumzo hayo kwa kuwashirikisha wananchi wote.
Rais Salva Kiir amesema: "Mimi kama kiongozi wa taifa, siwezi kukubali watu wa nchi hii waendelee kuteseka na kunyamaza kimya nikiona taifa likiporomoka."
Kadhalika katika hotuba hiyo kwa taifa, Rais Kiir ameomba msamaha kwa makosa ambayo huenda ameyafanya, bila kutaja moja kwa moja makosa yenyewe. Aidha amezitaka pande hasimu katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika, kuzika tofauti zao, kusitisha uadui na uhasama; na kusherehekea kwa pamoja sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.
Hii ni katika hali ambayo, hapo jana, Yasmin Sooka, Mjumbe wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, akizungumza katika kikao cha dharura cha baraza hilo mjini Geneva alisema iwapo jamii ya kimatifa inataka Sudan Kusini isitumbukie katika mauaji ya kimbari, basi sharti askari 4,000 wa kulinda amani watumwe nchini humo haraka iwezekanavyo; sambamba na kuundwa mahamaka maalumu ya kuwashtaki watenda jinai katika nchi hiyo.