Misri yailaumu vikali Qatar, (P) GCC yailalamikia serikali ya Cairo
Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imetoa taarifa ya kuilaumu tena Qatar na kuituhumu kuwa ilihusika katika tukio la kigaidi la mripuko uliotokea kwenye kanisa la Othodoksi la Saint Mark la Waqibti katika mji mkuu Cairo.
Kupitia taarifa yake iliyoelekeza tena kidole cha tuhuma kwa harakati ya Kiislamu ya Ikhwanul Muslimin ya kuhusika na mripuko uliolenga kanisa hilo, serikali ya Misri imetangaza kuwa kundi la Ikhwanul Muslimin ambalo wafuasi wake wanaishi nchini Qatar limefanya shambulio hilo ili kuzusha fitna, machafuko na kuvuruga utulivu nchini Misri.
Harakati ya Ikhwanul Muslimin imekanusha kuhusika kwa namna yoyote ile na shambulio hilo.
Hii ni katika hali ambayo hapo kabla Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (P)GCC Abdulatif Al- Zayyani alilalamikia tuhuma zilizotolewa na Misri dhidi ya Qatar za kuhusika na tukio la mripuko katika kanisa la Waqibti mjini Cairo ambapo watu 27 waliuawa na wengine 50 walijeruhiwa.
Kufuatia shambulio hilo la siku ya Jumapili ya tarehe 11 Desemba, Rais wa Misri Abdel Fattah el Sisi alitangaza siku tatu za maombolezo nchini humo.../