Waangalizi wa ndani Ghana waidhinisha matokeo ya uchaguzi wa Bunge na Rais
Waangalizi wa ndani katika uchaguzi uliopita wa Bunge na Rais katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika wameunga mkono na kuidhinisha matokeo ya uchaguzi huo.
Taarifa ya wasimamizi hao wa ndani wa uchaguzi sambamba na kuunga mkono matokeo ya uchaguzi huo imesisitiza kuwa, matokeo ya uchaguzi huo yameonesha irada na azma thabiti ya wananchi wa Ghana ya kujiainishia mustakbali wa kisiasa wa nchi yao.
Katika taarifa yake pia, Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa sanjari na kusifu kufanyika kwa mafanikio makubwa uchaguzi wa Ghana ametangaza himaya na uungaji mkono wake kwa serikali mpya ya nchi hiyo.
Kiongozi mkongwe wa upinzani nchini Ghana, Nana Akufo-Addo, aliibuka mshindi katika uchaguzi wa rais uliofanyika Desemba 7 mwezi huu na kumshinda Rais John Dramani Mahama wa chama tawala.
Mahama ambaye alishika hatamu za kuiongoza nchi hiyo Julai mwaka 2012 baada ya kuaga dunia Rais John Atta Mills na kisha kushinda katika uchaguzi mdogo wa 2013, amebwagwa na Nana Akufo-Addo wa chama cha New Patriotic NPP, ambaye alikuwa anawania kiti cha urais kwa mara ya tatu.
Ghana ni moja ya nchi chache za Afrika zenye kuheshimu misingi ya demokrasia na zenye historia ya kushuhudia mchakato wa amani wa kukabidhi madaraka kutoka serikali moja hadi nyingine.