UN yataka kutekelezwa makubaliano ya kukabidhi madaraka Kongo DR
(last modified Thu, 05 Jan 2017 07:56:44 GMT )
Jan 05, 2017 07:56 UTC
  • UN yataka kutekelezwa makubaliano ya kukabidhi madaraka Kongo DR

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetaka kutekelezwa kikamilifu makubaliano ya kukabidhi madaraka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema linataraji kuwa makubaliano hayo yatatekelezwa kikamilifu  bila ya uakhirishaji na kwa nia njema kabisa kwa mujibu wa katiba ya Kongo. Baraza la Usalama la UN pia limezitaka pande za kisiasa nchini humo ambazo hazikusaini makubaliano hayo ziyasaini haraka iwezekanavyo. Makubaliano ya kukabidhi madaraka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanaeleza kuwa, Kongo inapaswa kuongozwa kwa pamoja kati ya wapinzani na serikali baada ya kumalizika duru ya urais ya  Joseph Kabila na kuchaguliwa shakhsia mwingine atakayeiongoza nchi hiyo.

Raisi Joseph Kabila anayepasa kung'atuka madarakani mwishoni mwa mwaka huu 

Umoja wa Mataifa aidha umesisitiza kuhusu azma yake ya kuunga mkono utekelezaji wa makubaliano hayo kwa kushirikiana kwa karibu na Umoja wa Afrika na pia kufuatilia hali ya mambo ya Kongo DR kuhusu haki za binadamu. Nchi 15 wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimesisitiza kwa kauli moja umuhimu wa kufanyika uchaguzi wenye itibari kabla ya kumalizika mwaka huu; kwa mujibu wa pendekezo lililotolewa na Ufaransa.