Nchi za Afrika kuendelea kuwapa hifadhi wakimbizi wa Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22927-nchi_za_afrika_kuendelea_kuwapa_hifadhi_wakimbizi_wa_somalia
Nchi tano za pembe ya Afrika zinazohifadhi wakimbizi wa Somalia, zimesema zitaendelea kuwapatia hifadhi wakimbizi hao huku jamii ya kimataifa ikiendeleza harakati za kurejesha amani ya kudumu nchini mwao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 06, 2017 04:23 UTC
  • Nchi za Afrika kuendelea kuwapa hifadhi wakimbizi wa Somalia

Nchi tano za pembe ya Afrika zinazohifadhi wakimbizi wa Somalia, zimesema zitaendelea kuwapatia hifadhi wakimbizi hao huku jamii ya kimataifa ikiendeleza harakati za kurejesha amani ya kudumu nchini mwao.

Mohammed Abdi Affey ambaye ni mjumbe maalum wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR kwa wakimbizi wa Somalia, alizungumza na waandishi habari  mjini Geneva, Uswisi Alhamisi na kutoa ripoti ya ziara yake kwenye nchi zinazohifadhi wakimbizi wa Somalia kwa miaka 25 sasa.

Affey ametembelea Kenya, Yemen, Uganda, Djibouti, Ethiopia na Somalia akisema lengo ni kushawishi fursa zao za hifadhi zisibinywe, na kuongeza kuwa marais wa nchi hizo wamekubali kuendelea kuwalinda wakimbizi hao. Hata hivyo amesema kuna haja ya kuongeza maradufu jitihada za kuleta utulivu Somalia na usaidizi zaidi kwa wenyeji wanaohifadhi wakimbizi kwani hilo linapunguza msuguano kati ya wakimbizi na wenyeji.

 Alipoulizwa kuhusu wakimbizi wasio raia wa Somalia kwenye kambi ya Daadab nchini Kenya, Bwana Affey amesema serikali ya Kenya sasa imeanza kuwashughulikia raia wa Kenya walioingia kambini kwani wote wanatoka jirani na kambi hizo ambako kuna changamoto za maisha. Amesema  mchakato huo unafuatiliwa na serikali ya Somalia, Kenya na UNHCR.

Hivi karibuni idadi kubwa ya wakimbizi wa Kisomali waliorejeshwa kwa khiari nchini Somalia wamesema ahadi walizopewa kabla ya kurejeshwa nchini humo hazijatekelezwa na sasa baadhi yao wanataka kurejea katika kambi ya Dadaab nchini Kenya.

Serikali ya Kenya hivi karibuni ilitangaza mpango wa kuifunga kambi ya Dadaab kikamilifu kufikia mwezi Mei mwaka 2017 kutokana na sababu za kiusalama, kijamii na kiuchumi.