UN: Watu 28 wameuawa Libya mwaka huu 2016
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, watu 28 wamepoteza maisha na wengine 38 kujeruhiwa kwenye mapigano na ghasia katika maeneo mbalimbali ya Libya.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa jana imesema kuwa, wahanga wa ghasia hizo ni raia wasio na hatia. Ripoti hiyo pia imesema kutokana na mapigano kuhusisha makundi mengi na ukosefu wa njia salama za kutuma waangalizi wa kimataifa katika nchi hiyo, ni vigumu kubaini ni upande upi iliotekeleza mauaji hayo ya raia wasio na hatia. Ripoti ya Umoja wa Mataifa pia imesema wapiganaji wa makundi ya wanamgambo pamoja na wanajeshi wa serikali ambao idadi yao haijulikani pia wameuawa kwenye mapigano ya Libya tangu kuanza mwaka huu wa 2016.
Tangu kutekwa mji mkuu wa Libya, Tripoli mwaka 2104 na wapiganaji wa Fajr, nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na matatizo makubwa ya kisiasa na kiusalama. Kuna serikali mbili na mabunge mawili ambapo kila ipande unasisitiza kuwa ndio mwakilishi halali wa wananchi. Hata hivyo bunge na serikali zenye makao katika mji wa Tobruk mashariki mwa nchi ndizo zinazotambuliwa rasmi kimataifa.