Rais wa Afrika Kusini atoa wito wa kushikamana na wananchi wa Palestina
Rais wa Afrika Kusini ametoa mwito wa wananchi wa nchi hiyo kushikamana na kufungamana na wananchi wa Palestina.
Rais Jacob Zuma amesema hayo katika hotuba yake kwa mnasaba wa mwaka wa 105 wa kuasisiwa chama tawala nchini humo cha ANC na kusisitizia wajibu wa kushikamana chama chake na wananchi madhulumu wa Palestina. Rais Zuma amewataka wananchi wa Afrika Kusini kutotembelea ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kupachikwa jina la Israel ikiwa ni kuonyesha mshikamano na wananchi hao wa Palestina.
Rais wa Afrika Kusini amebainisha kwamba, wananchi wa Palestina ambao wanaendesha mapambano yao ya kupigania uhuru na mamlaka ya nchi yao wangali wanaendelea kukadhulumiwa na kukandamizwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Aidha Rais Zuma ameliunga mkono azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lililaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina na kuutaja ujenzi wa vitongoji hivyo kuwa ni haramu.
Rais wa Afrika Kusini amesisitizia pia udharura wa kukomeshwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina.
Katika miaka ya hivi karibuni serikali ya Afrika Kusini mara kadhaa imelaani siasa za kibaguzi za Israel dhidi ya wananchi wa Palestina na imepiga marufuku kuingizwa nchini humo bidhaa zilizotengenezwa huko Israel. Miongoni mwa siasa za serikali ya Rais Zuma ni kuwa, raia wa nchi hiyo anaruhusiwa kuwa na uraia wa nchi mbili lakini atapoteza uraia wa Afrika Kusini endapo uraia wake wa pili utakuwa ni Israel.