AU, EU na UN zataka kutatuliwa tofauti zilizopo jimbo la Galmudug, Somalia
Wawakilishi wa Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa wametaka kutatuliwa haraka tofauti zilizopo katika jimbo la Galmudug nchini Somalia kupitia njia ya mazungumzo.
Wawakilishi hao kwa kushirikiana na mabalozi wa kigeni waliopo nchini Somalia sambamba na kutoa wito huo, wameeleza wasiwasi wao kutokana na kuendelea tofauti kati ya jamii ya watu wa eneo hilo la katikati mwa Somalia na Abdikarim Guled, gavana wa jimbo hilo. Kufuatia ukosoaji wa wawakilishi wa Bunge juu ya uongozi mbaya wa Abdikarim Guled, siku ya Jumanne iliyopita gavana huyo aliuzuliwa baada ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye katika bunge hilo.
Kufuatia hali hiyo Ali Hared Ali, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Somalia alitangaza kuwa, jumla ya wabunge 54 walipiga kura ya kutokuwa na imani na kiongozi huyo na hivyo kumvua nafasi yake.
Abdikarim Guled aliteuliwa katika nafasi ya ugavana mwaka 2015; hata hivyo anatuhumiwa kwamba hana sifa za uongozi na kwamba amekuwa akitoweka mara kwa mara kazini.
Tofauti hizo zimekuwa kubwa kiasi cha kutishia kuibuka mapigano mapya eneo hilo. Kwa mujibu wa katiba, Mohamed Hashi Araby naibu gavana wa Galmudug ndiye aliyetakiwa kuchukua nafasi ya hiyo, huku Bunge nalo likitakiwa kumchagua gavana mwingine.