Azikiwe: Kuondolewa Sudan vikwazo na US ni malipo kwa kushirikiana na Saudia
Abayomi Azikiwe, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mwandishi wa habari wa kiafrika amesema kuwa, uamuzi wa serikali ya Marekani wa kuiondolea Sudan baadhi ya vikwazo ilivyokuwa imeiwekea ni malipo ya Khartoum baada ya kubadili msimamo wake kuhusu nchi za Magharibi na kuimarisha uhusiano wake na Saudi Arabia.
Azikiwe ambaye anaishi katika mji wa Detroit jimbo la Michigan nchini Marekani ameyasema hayo katika mahojiano aliyoyafanya na kanali ya televisheni ya Press TV na kuongeza kuwa, baada ya serikali ya Sudan kuboresha uhusiano wake na Saudia ambayo ni rafiki mkubwa wa Marekani, Washington ilichukua uamuzi wa kuitunuku nchi hiyo zawadi ya kuiondolea baadhi ya vikwazo.
Ameongeza kuwa, masuala kama vile kuungana na Saudia katika mashambulizi yake makali dhidi ya watu wa Yemen ambayo hadi sasa yameua maelfu ya watu wasio na hatia na kadhalika kukata uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni mambo ambayo yamewafurahisha mno viongozi wa Marekani na kuamua kuitunuku zawadi hiyo.
Abayomi Azikiwe amezidi kufafanua kwa kusema, ni suala lisilo na shaka kwamba, hatua ya Sudan kuondolewa baadhi ya vikwazo vya kiuchumi na Marekani ni malipo kwa Khartoum baada ya kujikurubisha kwa Wamagharibi na rafiki wao, Saudia.
Siku ya Ijumaa Rais Barack Obama wa Marekani alitoa amri ya kupunguzwa na hatimaye kuondolewa kikamilifu vikwazo ambavyo nchi yake imeiwekea Sudan. Katika barua aliyoiandikia Kongresi ya nchi hiyo, Obama ambaye uongozi wake umebakiwa na siku chache kumalizika, amedai kuwa, hatua chanya zilizochukuliwa na serikali ya Khartoum katika kipindi cha miezi sita iliyopita, ndizo zimeifanya serikali yake kuchukua maamuzi hayo.