Guterres ataka kuwekewa vikwazo wanaokiuka makubaliano ya amani Mali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i23734-guterres_ataka_kuwekewa_vikwazo_wanaokiuka_makubaliano_ya_amani_mali
Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa amelitaka Baraza la Usalama la umoja huo kuwawekea vikwazo wahusika wakuu wa ukiukaji makubaliano ya amani nchini Mali.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 17, 2017 04:22 UTC
  • Guterres ataka kuwekewa vikwazo wanaokiuka makubaliano ya amani Mali

Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa amelitaka Baraza la Usalama la umoja huo kuwawekea vikwazo wahusika wakuu wa ukiukaji makubaliano ya amani nchini Mali.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa UN aliyasema hayo jana katika ripoti iliyosambazwa kwa nchi wanachama wa Baraza la Usalama na kubainisha kuwa, makubaliano hayo ya amani ya mwaka 2015 kati ya serikali na makundi ya waasi yanatekelezwa kwa mwendo wa kinyonga.

Ripoti ya Guterres imefafanua kuwa: "Ingawaje hatua chache za utekelezwaji wa makubaliano hayo zimepigwa katika kipindi cha miezi 18 iliyopita, lakini mchakato wa amani nchini Mali upo katika hatua nyeti, na yeyote anayeashiria kuweka vizingiti lazima awekewe vikwazo." 

Wanajeshi wa MINUSMA wakishika doria nchini Mali

Serikali ya Mali na makundi yenye silaha ya wapinzani tarehe 15 Mei mwaka juzi 2015 yalisaini makubaliano ya amani baada ya duru kadhaa za mazungumzo kwa upatanishi wa Algeria.

Mwishoni mwa mwaka uliopita 2016, Umoja wa Mataifa ulisema kuwa kuongezeka hali ya mivutano kaskazini mwa Mali kunatishia makubaliano ya kusitisha mapigano nchini humo.

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali (MINUSMA) kimeyaonya makundi yenye silaha yaliyosaini makubaliano ya kusimamisha mapigano na kutahadharisha juu ya kuanza tena mapigano katika eneo la Kidal kaskazini mwa Mali.

Wapiganaji wa Mali