UN: Somalia inahitaji misaada ya dharura kukabiliana na njaa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i23869-un_somalia_inahitaji_misaada_ya_dharura_kukabiliana_na_njaa
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, imezindua ombi la dola milioni 864 kwa ajili ya kushughulikia mahitaji ya kibinadamu nchini Somalia kwa mwaka huu wa 2017.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 19, 2017 04:09 UTC
  • UN: Somalia inahitaji misaada ya dharura kukabiliana na njaa

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, imezindua ombi la dola milioni 864 kwa ajili ya kushughulikia mahitaji ya kibinadamu nchini Somalia kwa mwaka huu wa 2017.

Uzinduzi huo umefanyika katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu ukilenga kukwamua watu milioni 3.9 nchini humo wanaohitaji msaada wa dharura wa chakula.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Naibu mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Peter de Clercq amesema jamii ya kimataifa inapaswa kuimarisha usaidizi kwa wananchi wa Somalia. Ameongeza kuwa fedha hizo zikipatikana zitaendelea kuokoa maisha na kuimarisha mbinu za kuishi, kwani zitawapatia huduma za msingi na kuwaepusha watu walio hatarini zaidi.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa pia na spika wa bunge la Somalia, Mohamed Sheikh Osman Jawari, maafisa waandamizi wa Umoja wa Mataifa na wale wa kibalozi nchini Somalia.

Ombi hilo limetolewa wakati huu ambapo Somalia inakabiliwa na ukame mkubwa uliosababisha watu milioni tano sawa na asilimia 40 ya wananchi wa Somalia kukabiliwa na uhaba wa chakula.

Kwa ujumla watu milioni 5 wanahitaji misaada ya kibinadamu Somalia huku watoto 320,000 wakikabiliwa na utapiamlo shadidi na hivyo wanahitaji msaada wa dharura wa lishe bora.

Takwimu zinaonyesha kuwa kuna wakimbizi milioni 1.1 wa ndani ya nchi (IDP) kote Somalia ambao nao pia wanahitaji misaada mbali mbali ya dharura. Aidha watu wengine milioni 3.3 hawana huduma za dharura za afya huku wakihitajia maji safi ya kunywa na afya ya kijamii.