Gambia yasubiri rais mpya kuiongoza nchi
Hatimaye baada ya nchi kadhaa za magharibi mwa Afrika kutuma wanajeshi wake huko Gambia, Yahya Jammeh ametangaza kuondoka madarakani katika fursa ya mwisho.
Kwa mujibu wa katiba ya Gambia, Jammeh alipasa kuondoka madarakani kufikia tarehe 19 mwezi huu wa Januari na kisha kufanyika sherehe za kumuapisha Rais Mpya wa nchi hiyo Adama Barrow, hata hivyo kuendelea kung'ang'ania madarakani kiongozi huyo kumezipelekea nchi za Magharibi mwa Afrika kuanzisha hatua ya kijeshi na kutuma wanajeshi wao katika mpaka wa Senegal na Gambia ili kufuatilia tahadhari walizokuwa wametoa hapo kabla. Rais wa Mauritania aliwasili Banjul mji mkuu wa Gambia kwa ajili ya mashauriano ya mwisho na kisha akaelekea Senegal wakati wanajeshi hao wa nchi za Magharibi walipokuwa wakijiandaa kuwasili Gambia ili kumshinikiza Jammeh ang'atuke madarakani.
Rais Muhammad Ould Abdulaziz wa Mauritania ameeleza kuwa Rais Yahya Jammeh wa Gambia amesema kuwa ameamua kuondoka madarakani kwa amani. Hata kama Jammeh alifanya kila aliloweza ili aendelee kubaki madarakani kukiwemo kutangaza hali ya hatari, lakini inaonekana kuwa kuzidi kukabiliwa na upinzani, kukimbia nchi baadhi ya washirika wake wakuu wa kisiasa na muhimu zaidi hatua ya mkuu wa majeshi ya Gambia ya kutangaza kutokabiliana na vikosi vya Senegal ni sababu muhimu zilizomfanya Jammeh aamue kuondoka madarakani. Wakati huo huo sherehe za kumuapisha rais mpya wa nchi hiyo zimefanyika katika ubalozi wa Gambia huko Senegal.
Kwa mara nyingine tena sasa viongozi wa nchi mbalimbali za Magharibi mwa Afrika wanasubiri kuona madaraka ya kuiongoza Gambia yakikabidhiwa kwa rais mpya kwa njia ya amani na kisha rais huyo aanze kutekeleza majukumu yake. Hata kama Jammeh ametangaza kuwa ataondoka madarakani, lakini kungali kuwa wasiwasi wa iwapo ataheshimu uamuzi wake huo au la.
Kwa msingi huo wapatanishi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) na Umoja wa Afrika (AU) kwa mara nyingine wamemtahadharisha Jammeh na kumtaka ajiepushe kuchukua maamuzi yasiyo ya kimantiki ya kupoteza tu muda ambayo huenda yakaitumbukiza Gambia katika migogoro mikubwa ya kisiasa na kiuchumi kwa kuzingatia kuwa tayari vikosi vya nchi kadhaa za magharibi mwa Afrika vimtumwa katika mpaka wa nchi hiyo. Radiamali ya haraka iliyotolewa na nchi za magharibi mwa Afrika imeonyesha kuwa Umoja wa Afrika na taasisi nyingine kama Ecowas zina uwezo wa kutatua migogoro ya nchi za Kiafrika na hivyo kuzuia uingiliaji wa nchi ajinabi katika mambo ya ndani ya bara hilo.
Hatua ya Jammeh ya kukataa kuondoka madarakani imezipekekea nchi hizo zikaribie kuchua hatua ya kijeshi, hata hivyo hatari hiyo hivi sasa inaoonekana kuepukwa kwa kiwango fulani. Katika uongozi wake, Yahya Jammeh amekuwa akikandamiza uhuru wa kisiasa, kutumia mabavu na kuwatia mbaroni wapinzani ili aendelee kuwepo madarakani. Suala la kukabidhi madaraka kwa rais mpya limeleta matarajio mapya hivi sasa nchini humo. Adama Barrow ambaye anatambulika kuwa mmoja wa wafanyabiashara mashuhuri huko Gambia ameahidi kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa na kuboresha hali ya kisiasa na kiuchumi nchini humo. Hata kama ushindi wake haukutabiriwa, lakini sasa Adama Barrow ndiye rais rasmi wa nchi hiyo kutokana na kuchaguliwa kwa wingi wa kura za wananchi.