Jammeh wa Gambia hakupewa kinga ya kutoshtakiwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24107-jammeh_wa_gambia_hakupewa_kinga_ya_kutoshtakiwa
Viongozi wa nchi za Afrika Magharibi hawakuafiki kupewa kinga ya kutoshtakiwa aliyekuwa rais wa Gambia Yahya Jammeh wakati wa mazungumzo ya kumshawishi mtawala huyo wa miaka mingi kwenda uhamishoni baada ya kushindwa katika uchaguzi.
(last modified 2026-06-17T03:32:54+00:00 )
Jan 23, 2017 04:59 UTC
  •  Jammeh wa Gambia hakupewa kinga ya kutoshtakiwa

Viongozi wa nchi za Afrika Magharibi hawakuafiki kupewa kinga ya kutoshtakiwa aliyekuwa rais wa Gambia Yahya Jammeh wakati wa mazungumzo ya kumshawishi mtawala huyo wa miaka mingi kwenda uhamishoni baada ya kushindwa katika uchaguzi.

Viongozi wa nchi za Afrika Magharibi hawakuafiki kupewa kinga ya kutoshtakiwa aliyekuwa rais wa Gambia Yahya Jammeh wakati wa mazungumzo ya kumshawishi mtawala huyo wa miaka mingi kwenda uhamishoni baada ya kushindwa katika uchaguzi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Senegal, Mankeur Ndiaye amesema "Jammeh na timu yake wametayarisha taarifa ambayo inapaswa kuidhinishwa na Jumuiya ya Kiuchumi Magharibi mwa Afrika ECOWAS, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika ambayo kimsingi inampa kinga." Ndiaye amesema taarifa hiyo inakiuka utawala wa sheria na kwamba haijaidhinishwa na yeyote. 

Yahya Jammeh

Matamshi ya Ndiaye yanakuja baada ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kuchapisha taarifa ya pamoja ambayo imetajwa kuwa yenye lengo la kufikia suluhisho la amani kwa mgogoro wa kisiasa Gambia. Taarifa hiyo imeahidi kulinda haki za Jammeh kama raia, kiongozi wa chama cha kisiasa na rais wa zamani sambamba na kuzuia kuchukuliwa mali zake na za waitifaki wake na kuhakikisha kuwa hatimaye anarejea Gambia. Pamoja na hayo Waziri wa Mambo ya Nje wa Senegal amesema taarifa hiyo haijaidhiniswa na ECOWAS. Aidha amesema Rais mpya wa Gambia Adama Barrow, ambaye aliapishwa Alhamisi iliyopita katika ubalozi wa Gambia katika mji mkuu wa Senegal Dakar, naye pia hakujulishwa kuhusu taarifa hiyo kabla haijachapishwa.

Adama Barrow akila kiapo cha kuwa Rais mpya wa Gambia

Hayo yanajiri baada ya Barrow kusema serikali yake itaunda Tume ya Ukweli na Maridhiano itakayobeba jukumu la kuchunguza madai ya ukiukaji wa haki za binadamu ya serikali ya Jammeh katika utawala wake wa miaka 22. Barrow ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, ni mapema sana kusema iwapo Jammeh atafunguliwa mashtaka.

Baada ya kukubali kuachia ngazi na kukabidhi madaraka kwa njia ya amani, rais wa zamani wa Gambia, Yahya Jammeh ameenda uhamishoni nchini Equatorial Guinea.