Boko Haram yaendelea kutumia watoto kwenye hujuma zao Nigeria
Maafisa wa serikali ya Nigeria wameelezea wasi wasi wao kuhusu hatua ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Harm kukithirisha mbinu ya kutumia watoto wadogo katika harakati zao za kigaidi ikiwemo kutekeleza mashambulizi ya mabomu.
Ripoti mpya iliyochapishwa na shirika la habari la BBC na kunukuliwa na kanali ya televisheni ya Press TV ya Iran imefichua kuwa, wanachama wanawake wa kundi la magaidi wakufurishaji wa Boko Haram wanawatumia watoto wadogo katika upelelezi wao sambamba na kutekeleza hujuma za kigaidi.
Ripoti hiyo iliyotolewa na maafisa wa serikali ya Nigeria imebainisha kuwa, kutumiwa watoto wadogo katika mashambulizi ya kujitolea muhanga ya kigaidi kumekithiri sana nchini humo, jambo ambalo linawatia wasi wasi mkubwa.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, kundi la Boko Haram katika hujuma zake za hivi karibuni limewatumia zaidi, wanawake na watoto wadogo na kwamba mbinu hii imekuwa ikifanikiwa kwa kuwa wanawake na watoto wadodo ni wepesi wa kuepuka vizuizi vya maafisa usalama sambamba na kujipenyeza kwenye mijumuiko na halaiki za watu pasina kushukiwa kuwa wahalifu.
Hii ni katika hali ambayo, Toby Lanzer, Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la magharibi mwa Afrika amesema kuwa, harakati za Boko Haram zimewaweka watoto nusu milioni wa kanda hiyo katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na lishe duni.
Mwezi Aprili mwaka jana, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (UNICEF) lilisema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita Boko Haram wameongeza mara 11 idadi ya watoto wanaotumiwa kufanya hujuma za kigaidi nchini Nigeria na pia katika nchi jirani za Cameroon, Chad na Nigeria.