Umoja wa Mataifa: Vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu DRC vimeongezeka
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu vimeongezeka mno katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa, katika mwaka uliopita wa 2016, vitendo vya ukiukaji haki za binadamu viliongezeka kwa asilimia 30 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake yaaani wa 2015.
Ofisi ya masuala ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa, katika mwaka uliopita kulisajiliwa matukio 5,190 ya ukiukaji wa haki za binadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa, zaidi ya asilimia 60 ya vitendo hivyo vya ukiukaji wa haki za binadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vinahusishwa na maafisa wa serikali na kikosi cha polisi.
Aidha ripoti hiyo imesisitiza kuwa, makundi ya wabeba silaha yamehusika na vifo vya watu 78 katika nchi hiyo mwaka uliopita na kwamba, asilimia 36 ya vitendo vya ukikaji wa haki za binadamu vilifanywa na makundi hayo ya wabeba silaha.
Sehemu nyingine ya ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa, wahanga wakuu wa vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni wapinzani wa kisiasa, wajumbe wa mashirika ya kiraia na waandishi wa habari.