Igad yaalani mashambulizi ya kundi la al Shabab, Somalia
Jumuiya ya Kieneo ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) imelaani mashambulizi ya kundi la wanamgambo wa al Shabab katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Jumuiya ya Igad imetoa taarifa ikilaani mashambulizi ya juzi ya kundi la al Shabab huko Mogadishu na kusisitiza kwa mara nyingine tena azma yakei ya kuunga mkono hatua yoyote ya kurejesha amani na utulivu nchini Somalia.
Milipuko miwili ya juzi iliyotokeka baada ya malori mawili yaliyotegwa mabomu kulipuka katika hoteli ya Dayah karibu na Bunge na Ikulu ya Rais mjini Mogadishu, imeuwa watu 32 na kujeruhi wengine 51.
Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) pia jana kilitangaza habari ya kuuawa magaidi tisa wa al Shabab katika shambulio lililofeli dhidi ya kituo cha polisi katika mji wa Afgoye kusini mwa Mogadishu, masaa kadhaa baada ya kulipuka malori mawili yaliyotegwa mabomu ndani yake huko Mogadishu.
Kundi la kigaidi la al Shabab ambalo tangu mwaka 2007 linapigana na kufanya hujuma mbalimbali ili kuing'oa madarakani serikali ya Somalia mwaka 2011 lilipoteza udhibiti wa mji mkuu na wa baadhi ya ngme zake zingine kama vile mji wa Afgoye. Kundi hilo limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika mji mkuu, Mogadishu.