Nigeria: Hatuungi mkono wazo la nchi za Afrika kujiondoa ICC kwa pamoja
Serikali ya Nigeria imesema haiungi mkono pendekezo linalotaka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika AU kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kwa pamoja.
Geoffrey Onyeama, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Nigeria amesema kuwa, serikali ya Abuja haiungi mkono stratejia hiyo inayotaka kutumiwa na AU akifafanua kuwa, kila nchi ina uhuru wa kuchukua uamuzi wake wa kibinafsi kuhusu kadhia hiyo na kwa khiari.
Amesema Nigeria, Senegal na Cape Verde ni baadhi ya nchi zinazopinga mpango huo wa Umoja wa Afrika akisisitiza kuwa, nchi wanachama wa AU zinahitaji muda zaidi kutathmini mapendekezo ya kamati iliyoundwa na umoja huo kupiga msasa na kuandaa mkakati wa pamoja wa kujiondoa kwa pamoja ICC, wanachama wa AU.
Amebainisha kuwa, Zambia, Tanzania, Liberia na Botswana tayari zimetangaza msimamo wao wa kutojiondoa kwenye Mkataba wa Roma uliounda ICC na hivyo haingii akilini kuzilazimisha nchi zote wanachama wa Umoja wa Afrika kujiondoa.
Tayari Gambia, Afrika Kusini na Burundi zimeanzisha mchakato wa kujiondoa katika Mkataba wa Roma kutokana na kile viongozi wa nchi hizo sawa na viongozi wengine wa Kiafrika wanakitaja kuwa, ICC kuwasakama tu viongozi wa nchi za bara hilo, huku ikifumbia macho jinai zinazofanywa na viongozi wa Magharibi. Aidha Kenya, Uganda na Namibia zimeashiria kuwa yumkini nazo zikajiunga na mkondo huo wa kujiondoa ICC.
Mwezi uliopita, Zeid Ra'ad al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alieleza wasiwasi wake kuhusu mwenendo wa kujiondoa nchi mbalimbali katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), na kueleza kuwa, hatua hiyo ni kuwasaliti wahanga wa ukiukwaji wa haki za binadamu.