UN: Somalia inakabiliwa baa la njaa, hatua za dharura zichukuliwe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24647-un_somalia_inakabiliwa_baa_la_njaa_hatua_za_dharura_zichukuliwe
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema, hali ya kibinadamu nchini Somalia imekuwa mbaya zaidi na kwamba kuna wasiwasi wa kutokea baa la njaa kwenye nchi hiyo mwaka huu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 03, 2017 10:40 UTC
  • UN:  Somalia inakabiliwa baa la njaa, hatua za dharura zichukuliwe

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema, hali ya kibinadamu nchini Somalia imekuwa mbaya zaidi na kwamba kuna wasiwasi wa kutokea baa la njaa kwenye nchi hiyo mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Dujarric amesema Ofisi ya Masuala ya Kibinadamu ya Umoja huo (OCHA) imesema, idadi ya watu wanaohitaji msaada nchini Somalia imeongezeka na kufikia milioni 6.2.

Amesema kiwango cha utapiamlo kimeendelea kuwa juu ambapo watoto laki 3.6 wenye umri wa chini ya miaka mitano wanakabiliwa na utapiamlo, kati yao elfu 71 wakiwa na utapiamlo mkali na wanakabiliwa na tishio la kupata magonjwa na hata kifo.

Aidha ripoti ya Shirika la Chakula Duniani FAO iliyozinduliwa Nairobi mji mkuu wa Kenya imeonyesha kuwa, maeneo mengi ya Somalia yana ukame na kwamba watu zaidi ya milioni sita wanakabiliwa na njaa kila siku.

Eneo la kugawa misaada ya chakula Somalia

Dick Trenchard, mwakilishi wa FAO  nchini Somalia ameonya kuwa maelfu ya watu wataaga dunia kutokana na njaa iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa za kuwafikishia misaada watu wanaokabiliwa na njaa katika nchi hiyo iliyokumbwa na kiangaiza huku vita vya wenywe kwa wenyewe vikiendelea.

FAO inasema, kwa ujumla ukame uliolikumba eneo la Pembe ya Afrika unatishia usalama wa chakula kwa watu wapatao milioni 17.

Kwa mujibu wa tangazo hilo la FAO,  mvua ya kiwango cha chini ilinyesha kati ya miezi ya Oktoba na Disemba mwaka jana na kwamba uchache huo wa mvua umesababisha mavuno hafifu na kupungua mifugo katika eneo la Pembe ya Afrika.