Mamia ya raia wa Sudan Kusini wakimbilia Uganda kila siku
Mamia ya raia wa Sudan Kusini wanakimbilia nchini Uganda kila siku kukimbia mapigano ya kikabila nchini mwao.
Shirika la habari la IRIB limeripoti habari hiyo na kumnukuu Luka Nyombe David, Kamishna eneo la Kajo Keji la kusini mashariki mwa Sudan Kusini akisema jana (Ijumaa) kwamba wimbi la machafuko mapya limepelekea mamia ya raia wa nchi hiyo wakimbilie nchi jirani ya Uganda kila siku.
Amesema, hali katika eneo hilo la mpakani ni tulivu kikamilifu hivi sasa lakini wakazi wa eneo hilo wanaendelea kukimbilia nchi jirani.
Wakati huo huo Charlie Paxley, msemaji wa Kamishna Mkuu wa Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa nchini Uganda amesema kuwa, makundi ya watu wenye silaha wanashambulia eneo la Kajo Keji kila siku wakichoma moto maeneo ya wakazi wa eneo hilo pamoja na kuwanajisi wanawake na watoto wadogo.
Sudan Kusini ilitumbukia kwenye mapigano ya ndani mwezi Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kumtuhumu makamu wake Riek Machar kuwa anafanya njama za kumpindua.
Mwezi Agosti 2015 pande hizo mbili zilifikia makubaliano ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na kukomesha mapigano ya ndani, hata hivyo makubaliano hayo yalivunjika mwezi Julai 2016 baada ya kuzuka mapigano huko Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini baina ya pande hizo mbili.
Makumi ya maelfu ya wananchi wa Sudan Kusini wameshauawa tangu mwaka 2013 na zaidi ya milioni mbili wengine wamekuwa wakimbizi. Si hayo tu, lakini pia, watu milioni nne na laki sita wa Sudan Kusini hawana usalama wa chakula.